MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu
Hassan amesema Tanzania imepiga hatua kubwa dhidi ya vita vya rushwa na
kuwataka waliokuwa wakisema kuwa nchi hii haiwezi kudhibiti rushwa waje
waone.
Alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya maadili na haki za
binadamu nchini viwanja vya Mwalimu Nyerere mjini hapa. Alisema
Tanzania imeshika nafasi ya 16 bora Afrika kwa upambanaji na rushwa
jambo ambalo linatia moyo kushuka kwa rushwa.
“Waliosema Tanzania hawawezi kudhibiti rushwa waje watutazame,”
alisema. Pia aliwataka wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa
vitendo vya na jitihada za Serikali kuziba mianya ya upotevu wa
rasilimali za nchi, mapato na mapambano dhidi ya rushwa.
Alisema lengo ni kuunganisha nguvu ya pamoja kusimamia maadili ya
taifa na utawala bora. Alisema ajenda kubwa duniani kwa sasa ni kuhusu
mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha utawala bora unaobeba mambo
mengi muhimu kama utawala wa sheria, haki za binadamu, maadili, uwazi na
uwajibikaji.
Alisema Serikali imekusudia kuona Tanzania inapata maendeleo kwa
manufaa ya wananchi. “Kufikia azma hii si suala dogo. Lazima wananchi na
Serikali kwa ujumla kujizatiti kutekeleza dira ya maendeleo ya taifa ya
2025 na ilani ya uchaguzi ya chama tawala 2015/2020 inayolenga
kuiwezesha nchi yetu kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda,"
alisema.
Alisema juhudi hizo haziwezi kufanikiwa wasipodhibiti rushwa na
kusimamia uadilifu na uwajibikaji ipasavyo. "Hatutasita kuwachukulia
hatua wale wote watakaotukwamisha kufikia azma hiyo," alisema Mama
Samia.
Alisema vita dhidi ya ukiukwaji wa maadili haviwezi kupiganwa na
Serikali peke yake ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha rushwa,
ubadhirifu na maovu mengine vinatokomezwa.
"Ni vyema tukahimizana suala la kuzingatia maadili na haki za
binadamu ili kufikia malengo ya kuwa taifa la mfano duniani, matatizo
yanayowakabili Serikali ni pamoja na matumizi mabaya ya nyaraka za siri
za Serikali,” alisema.
Alisema kukabiliana na changamoto ya maadili nchini Serikali
itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kisera na kisheria ambayo
itahakikisha vijana wanakuzwa kimaadili kwani hakuna taifa duniani
linaloweza kupata maendeleo bila utamaduni unaozingatia maadili.
"Kuna mtindo wa baadhi ya ofisi za Serikali kufanya kazi zao bila
kufuata utaratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya huduma kwa wateja na
dhamira ya Serikali ya kutoa huduma bora, hali hii inayotokana na
kuchukua muda mrefu kutekeleza wajibu wao au kurudisha mrejesho kwa
wananchi na hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi.
Alisema huduma zinazotolewa ni vyema zikaainishwa bayana muda
utakaotumika na vigezo vinavyohitajika. "Serikali hii inataka viongozi
wanaotimiza wajibu wao kwa wakati, vijana wenye mioyo na ari ya kazi
hivyo kama kuna mtu mzembe viongozi msisite kuwaondoa,” alisema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini
(Takukuru), Dk Valentino Mlowola alisema watatekeleza maagizo yote
yaliyotolewa kwani kwa kufanya hivyo wananchi wanajenga imani na
Serikali.
No comments