JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema shambulizi lililotokea
Desemba 7, mwaka huu dhidi ya askari wake wanaolinda amani Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni baya na halijawahi kutokea tangu vikosi
vyake vianze kushiriki Ulinzi wa Amani huko kupitia Umoja wa Mataifa
mwaka 2011.
Kutokana na shambulio hilo lililodumu kwa saa 13, JWTZ imepoteza
askari 14 na wengine 44 wamejeruhiwa, wawili wakiwa hawajulikani walipo
na jitihada za kuwatafuta zinaendelea.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni
Jenerali James Mwakibolwa alisema shambulio lililotokea DRC ni shambulio
ambalo kwa mara ya kwanza jeshi hilo liliamua kutoa taarifa. Alisema
shambulio hilo limeleta madhara makubwa lakini kikosi chao kilichopo
huko bado kina uwezo wa kutekeleza majukumu kwa uhodari, ushupavu,
weledi na umahiri stahiki.
“Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la
ulinzi wa amani nchini DRC, Tutawakumbuka daima mashujaa wetu hao,”
alisema Kamanda huyo. Alisema taratibu za kusafirisha miili ya marehemu
kuirejesha nchini zinafanyika chini ya utaratibu wa Serikali na Umoja wa
Mataifa. Alisema taratibu za kuwajulisha familia za wafiwa zimekamilika
ndiyo maana hawakuweza kutoa taarifa hizo bila kuweka sawa familia zao.
Alisema kutokana na shambulio hilo, JWTZ na Serikali zinaendelea
kuchukua hatua stahiki ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika.
“Kwa umoja wetu Watanzania tuombee dua roho za mashujaa wetu zipumzike
kwa amani na majeruhi wetu wapone haraka iwezekanavyo ili warejee
kutekeleza majukumu yao,” alisema.
Desemba 07, mwaka huu jioni sehemu ya Kikosi cha askari wa JWTZ
kilichopo DRC kulinda amani kilivamiwa na waasi wa kundi la Allied
Democratic Forces (ADF) katika kambi ndogo iliyopo eneo la daraja mto
Simulike barabara ya kutokea Oicha kwenda Kamango mpakani mwa Uganda
Kaskazini Mashariki ya Wilaya ya Beni, jimbo la Kivu Kaskazini. Hata
hivyo, shambulio hilo la kuvizia lilizusha mapigano baina ya kikosi cha
JWTZ na waasi hao ambapo askari wa JWTZ waliuawa na wengine kujeruhiwa
vibaya. UN imethibitisha.
No comments