MAHAKAMA
mkoani Tabora imemhukumu Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani
Tabora ASP Bhoke Jullius Bruno na wenzake saba kwenda jela miaka 15
baada ya kupatikana na hatia kwa makosa matatu yaliyokuwa yakiwakabili
ya kupanga njama ,kuiba silaha (bunduki 8 aina ya SMG na kushindwa
kuzuia wizi huo .
Bhoke na wenzake CPL Idd Abdalah, PC Mwinyi Gonga na Said Mgonela
aliyekuwa muhudumu waliokuwa wajiriwa wa jeshi la polisi upande wa
kikosi cha kutuliza ghasia walikuwa wanakabiliwa na tuhuma tatu ikiwemo
ya wizi wa bunduki nane aina ya SMG mali ya mwajiri wake.
Wengine waliopewa adhabu hiyo na Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda
ya Tabora, Sharmira Sarwatt ambaye alisikiliza shauri hilo ni Shaban
Haruna, Shaban Kabanika na Idd Supu. Akitoa hukumu hiyo Sarwatt alisema
kuwa ni maoni ya mahakama hiyo kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha
pasiposhaka makosa hayo na inawatia hatiani washitakiwa saba kati ya
kumi.
Sarwatt alisema katika hukumu hiyo kuwa ushahidi umeonyesha kuwa
mshitakiwa wa kwanza hadi wa tatu ambao walikuwa ni waajiriwa wa jeshi
la polisi walihusika katika makosa yote matatu ya kula njama, kuiba na
kushindwa kuzuia tukio.
Aliongeza kuwa hakuna ubishi kwamba silaha hizo zilipotea, zilikuwa
zikitunzwa ghalani, kibali kiliombwa kwa ajili ya kwenda kuzifanyia
matengenezo na kwamba mbili kati ya hizo zilipatikana moja Mbagala na
nyingine Sikonge.
Alisema kuwa kuiba silaha za jeshi ambazo zingetumika kulinda raia na
mali zake si kitendo ambacho mahakama inakifuraia. Aliongeza kuwa
mahakama imechukulia uzito wa makosa ya wizi wa silaha za jeshi hivyo
inajukumu la kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili liwe funzo kwao na
kwa jamii yenye tabia kama hizo ndipo akawahukumu kwenda jela miaka
mitano kwa kila kosa.
Awali upande wa serikali ukiongozwa na wakili mwandamizi Juma Masanja
aliiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo kati
ya mwezi Aprili 2013 na April 2014.
Ilidaiwa katika shitaka la kwanza kuwa katika tarehe tofauti
washitakiwa walikula njama ya kuiba bunduki aina ya SMG mahali ambapo
zilikuwa zimehifadhiwa katika ghala la kituo cha kutuliza ghasia cha
mjini Tabora.
Upande wa mashitaka ulidai katika shitaka la pili kuwa katika kipindi
hicho washitakiwa kwa pamoja bila kuwa na haki ya kuchukua silaha
kwenye kituo cha FFU Tabora waliiba bunduki nane aina ya SMG.
Wakili Masanja alidai kuwa watuhumiwa wakiwa watumishi FFU Tabora
walishindwa kutumia njia za kiusalama katika utunzaji wa silaha matokeo
yake bunduki nane aina ya SMG ziliingia katika mikono ya watu
wasioaminiwa na serikali.
Washitakiwa wengine watatu ambao walioachiliwa na mahakama baada ya
kukoseka ushahidi wa kuwatia hatiani ni Charles Abiud, Emanuel Festo na
Nicholaus Mlelwa. Upande wa utetezi katika shauri hilo namba 104/2015
uliwakilishwa na mwakili wasomi Kelvin Kayaga na Mussa Kassim.
No comments