RAIS John Magufuli ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuchukua hatua
dhidi ya vyombo vya habari vinavyotangaza muziki wakati wachezaji wakiwa
wako nusu uchi.
Mbali na kuitaka Wizara na TCRA kuchukua hatua, Rais Magufuli pia
aliitaka Jumuiya ya Wazazi kusimamia maadili ya Watanzania yaliyoanza
kutoweka taratibu. Aliyasema hayo wakati akiwahutubia wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa Tisa wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Tanzania alioufungua mjini
Dodoma jana.
Rais Magufuli alisema kuwa yeye ni shabiki mzuri wa muziki, lakini
cha kusikitisha kila anapofungua muziki, wanaoonekana kucheza wakiwa
utupu ni wanawake na siyo wanaume. Alisema miziki ya aina hiyo inaharibu
maadili ya watoto na siyo lazima iwe ndiyo miziki pekee ya kuchezwa.
Alisema umefika wakati kwa Watanzania bila kujali tofauti zao za
kiitikadi, wayalinde maadili yao ya Kitanzania. Alisema maadili ya ku
‘copy’ na ku ‘paste’ yatalipeleka Taifa kubaya. “Kwa nini uwavulie watu
wengine utupu wako?
Tena siyo kwa wakati muafaka? Niwaombe Jumuiya ya Wazazi, kila
kinachotokea ambacho kinaenda tofauti na maadili ya Kitanzania, hata
kama tunashindwa kuchukua hatua, basi tupige kelele; kelele zetu watu
watazisikia na Mungu atazisikia,”alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, enzi za akina Mama Maria Nyerere na
Fatma Karume mambo hayakuwa hivi kama leo na kukishangaa kizazi cha sasa
kimekumbwa na mdudu gani. Alisema imekuwa vigumu kwa familia kukaa
pamoja na kuangalia vipindi vya muziki kwenye televisheni kwa kuwa mambo
yanayofanyika hapo ni aibu.
Alisema Jumuiya ya Wazazi ina wajibu mkubwa wa kukemea uovu huo
unaovunja tabia njema za Watanzaia. Aidha, alivishangaa vyombo na wizara
vinavyohusika kusimamia maadili nchini kukaa kimya wakati mambo hayo
yakiendelea kuharibu maadili ya Watanzania.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria Mkutano huo wa Jumuiya ya Wazazi ni
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
viongozi wastaafu wa Chama na Serikali, viongozi wa upinzani pamoja na
Mama Maria Nyerere.
No comments