Heade

MAAGIZO YA MAJALIWA YAENDELEA KUTIKISA MKOA WA MARA

NAIBU Waziri Ofi si ya Rais TAMISEMI, Josephat Kandege ameagiza kuvunjwa kwa mkataba wa Sh bilioni 3.2 kwa ajili ya ujenzi wa ofi si ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara, iliyokuwa ikijengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Kandege ametoa agizo hilo baada ya kufanya ukaguzi na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Hivi karibuni akiwa ziarani Butiama, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia na Rushwa (Takukuru), kumkamata na kumhoji Meneja wa Mkoa wa TBA, Peter Salim baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi huo.
Mbali na hilo, Majaliwa pia alimuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kutokana na kuwapo tabia ya kutumia fedha za miradi ya maendeleo katika shughuli nyingine, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Pia aliagiza kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Solomon Ngiliule, Mweka Hazina wa Halmashauri, Masanja Sabuni na Ofisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo, Robert Makendo. Ili kuhakikisha kazi ya uchunguzi inafanyika haraka, Majaliwa alimwagiza Naibu Waziri, Kandege, kubaki Butiama ili kuhakikisha ukaguzi huo maalumu unafanyika juu ya fedha zinazotumwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa halmashauri hiyo.
Akifafanua, Kandege alisema katika ukaguzi wake, amebaini kuwepo kwa kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo na utekelezaji wa mradi huo kufanyika eneo tofauti na lile la awali, ambalo lilikuwa limefanyiwa usanifu, jambo ambalo limeiongezea serikali gharama ya Sh milioni 180.
Aliongeza kuwa taarifa iliyotolewa na Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Mara kwa Waziri Mkuu ilieleza kuwa Sh milioni 400 kati ya Sh milioni 600, zilizopokelewa Aprili mwaka jana kutoka Serikali kuu, zimetumika kujenga msingi na kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 60, tofauti na hali aliyoikuta alipotembelea eneo hilo la mradi.
“Nimeshangazwa kuona hakuna msingi wowote uliojengwa mpaka sasa katika eneo la mradi, kwa hali hii mtendaji huyu wa TBA ametoa taarifa ya uongo kwa Waziri Mkuu “ Kwa kuzingatia makosa hayo yote, Serikali inaagiza kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi wa ofisi za halmashauri uliokuwa utekelezwe na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushindwa kutekeleza mradi huu kwa wakati, kuongeza gharama za mradi kinyume cha taratibu bila kupata kibali cha Baraza la Madiwani na Ofisi ya Rais TAMISEMI sambamba na kutoa taarifa za uongo kwa Waziri Mkuu” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kandege, kandarasi hiyo imesitishwa hadi hapo serikali itakapotoa maelekezo mengineyo. Kandege alikuwa ameambatana na Waziri Mkuu katika ziara ya siku saba mkoani Mara na mpaka sasa bado anaendelea na ufuatiliaji wa maagizo yote, yaliyotolewa na Waziri Mkuu wakati wa ziara hiyo.

No comments

Powered by Blogger.