Heade

ODINGA AJIAPISHA ,RAIS KENYATTA AREJEA

Kiongozi wa Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA) nchini Kenya, Raila Odinga amejiapisha kama ‘Rais wa Watu wa Kenya” mbele ya maelfu ya wafuasi wake wa NASA.
Tukio hilo la aina yake lilifanyika Uwanja wa Uhuru Park, Nairobi, miezi mitatu tu tangu Odinga adai kuibiwa kura katika uchaguzi mkuu uliopita. “Mimi, Raila Amolo Odinga, naapa kwamba nitalilinda taifa kama rais wa watu, Mungu nisaidie,” aliapa mbele ya umati uliomzunguka. Aliapishwa kiapo hicho na Mbunge wa Ruaraka, ambaye pia ni Wakili wa Kujitegemea, TJ Kajwang aliyesema haogopi kitakachompata kwa hatua yake hiyo.
Hata hivyo, wakati Odinga akiapa viongozi wengine wakuu wa chama cha Nasa, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula hawakuhudhuria sherehe hiyo. Odinga aliwaambia wafuasi wake kuwa viongozi hao hawakuwepo hapo kwa sababu watakazoelezwa baadaye, ingawa alisema wako pamoja naye katika hilo. Ilielezwa mapema jana, Polisi walitumia mabomu ya machozi, kuwatawanya maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika katikati ya Jiji la Nairobi, kusherehekea kuapishwa kwa Odinga. Odinga alinukuliwa akidai ndiye mwenye haki ya kuwa rais na siyo Rais Uhuru Kenyatta (pichani).
Odinga alishindwa kwenye uchaguzi wa rais Agosti 8 mwaka jana. Uchaguzi huo baadaye ulifutwa na Mahakama ya Juu baada ya Odinga kulalamika kutaka utenguliwe matokeo. Uchaguzi wa marudio ulifanyika mwezi Oktoba 25, 2017, lakini Odinga aliususia akidai usingekuwa huru na wa haki. Baada ya kugomea uchaguzi huo wa marudio, Rais Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura zaidi ya asilimia 98 ya kura, hivyo kuwa Rais kwa muhula wa pili na mwisho.
Kitendo hicho cha Odinga kuapishwa jana kama rais wa wananchi, kimeelezwa kinaweza kuleta mgogoro wa kikatiba na hali ya sintofahamu. Ilidaiwa wiki iliyopita NASA walitoa matokeo mengine ya uchaguzi uliopita wa Agosti, wakidai yalimpa ushindi Odinga na kudai wangeyatumia matokeo hayo kama sababu ya msingi ya kuapishwa kwake jana. Hata hivyo, matokeo hayo yalipingwa na Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) iliyosema si halali. Mapema jana, Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) ilivifungia vituo vitatu vya televisheni, kufuatia tukio la kuapishwa kwa Odinga.
Kituo cha kwanza kufungiwa na Mamlaka hiyo kilikuwa NTV kinachomilikiwa na Nation Media Group (NMG). Kituo kingine cha televisheni kilichofungiwa ni Citizen na baadaye kikafuata kituo cha televisheni cha KTN.
“Hakukuwa na taarifa yoyote rasmi juu ya hatua iliyochukuliwa ya kufungiwa kwetu. Tunaendelea kuwasiliana na mamlaka husika za serikali ili kujua sababu ya kufungiwa kwetu. Tunatumaini matangazo yatarudi tena muda siyo mrefu,” alieleza Mkurugenzi Mtendaji wa Vyombo vya Habari vya Royal, Waruru Wachira. Wakati huo huo, Rais Kenyatta alirejea nchini jana kutoka Ethiopia alikokwenda kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika.

No comments

Powered by Blogger.