Heade

TANZANIA NA MISRI WAANZA MKUTANO WA PAMOJA

Maofisa waandamizi na wataalamu kutoka sekta mbalimbali wa Tanzania na Misri, wameanza mkutano wa siku mbili wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) unaofanyika Misri kujadili mfumo wa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo.

Mkutano huo unaandaa misingi ya mkutano wa tatu mawaziri wa JPC utakaohitimishwa kwa kutiliana saini makubaliano mbalimbali katika sekta za kijamii na kiuchumi Jumatano hii.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Adolph Mkenda, aliuambia mkutano huo jana kuwa, ushirikiano wa kidugu baina ya Tanzania na Misri uliodumu kwa zaidi ya miongo mitano unahitaji kutiliwa mkazo zaidi katika masuala ya kiuchumi.

Profesa Mkenda anayeongoza ujumbe wa Watanzania katika mkutano wa wataalamu, alisema inafurahisha kuwa ingawa JPC haijakutana kwa miaka 20 iliyopita, nchi hizi zimeendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje kwa Afrika wa Misri, Balozi Mohamed Edrees alisema hiyo inathamini uhusiano wa dhati na Tanzania kusisitiza umuhimu wa kuuimarisha kwa kadiri inavyowezekana.

Alisema mazungumzo baina ya Rais John Magufuli na mwenzake alipozuru Tanzania Agosti 2017, yalionesha kuwa kujitoa walikokuonesha viongozi hawa kumeimarisha uhusiano na ushirikiano.

Alizipongeza juhudi za Tanzania kurejesha na kudumisha amani barani Afrika hususani Burundi na Libya huku akizisifu juhudi zinazofanywa na marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete katika mchakato wa amani katika nchiza Burundi na Libya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga, anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Watanzania katika mkutano wa mawaziri kesho. Baadhi ya wajumbe wa Tanzania ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Geberal Issa Nassor, Katibu Mkuu wa Tume ya Mipango ya Zanzibar, Juma Hassan Reli na Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Emmanuel Kalobelo.

Tanzania na Misri zimeendeleza uhusiano wa kidiplomasia tangu Juni 1964. Nchi hizi zinashirikiana katika Nyanja mbalimbali zikiwamo za kilimo, biashara, elimu, afya, maji, utalii, diplomasia, taarifa, utamaduni na michezo.

No comments

Powered by Blogger.