Heade

WANAOVAA NGUO ZISIZOKUWA NA MAADILI WATAONA CHA MTEMA KUNI

JESHI la Polisi limetangaza kufanya msako mkali kwa watu wanaovaa nguo zisizo na heshima, kulingana na maadili ya Tanzania na kuwafi kisha mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, wakati akitoa taarifa ya hali ya usalama kwa mwaka jana, alisema hivi sasa kuna wimbi la mavazi yasiyo sahihi wanayovaa baadhi ya watu.

“Hizi nguo hazipendezi na si maadili yetu, mnaiga wenzenu wanaovaa kwa sababu ya hali ya hewa ya kwao, sasa tunatangaza kuanza msako mwaka huu na tutakayemkamata tunamchukua hivyo hivyo hadi mahakamani bila kumpa nguo ya kujifunika, ili ndugu zako wakuone,” alisema.

Mkumbo aligusia pia kuongezeka kwa matukio ya kubaka na kulawiti, tofauti na matukio mengine ambayo yamepungua sababu ya jitihada za jeshi hilo kutoa elimu kwa wananchi.
 Alisema matukio ya kubaka kwa mwaka 2016 yalikuwa 144, ambapo mwaka 2017 yaliongezeka hadi kufikia 149, huku makosa ya kulawiti yakiongezeka kutoka 58 mwaka 2016 hadi 62 mwaka 2017.

Alisema sababu kubwa ya kuongezeka kwa makosa hayo ni sababu ya mila potofu, imani za waganga wa kienyeji na ukosefu wa elimu. Aidha, alisema ni vema kila Mtanzania akafahamu makosa hayo, hayafai na yana adhabu kubwa ya kifungo cha miaka 30 au maisha jela.

Alisema wakati matukio hayo, yakiongezeka matukio ya kiuhalifu wa aina mbalimbali, yamepungua kutoka 2,817 mwaka 2016 hadi kufikia matukio 1,963 mwaka 2017.
 Alisema Polisi wamefanikiwa kupunguza makosa hayo kutoka 854 sawa na asilimia 17.9 na kuomba wananchi kuendelea kulinda amani ya mkoa huo ili maendeleo ya kiuchumi waweze kuyapata.

No comments

Powered by Blogger.