Heade

DODOMA WAPATA TIBA YA KUPOROMOKA KWA ELIMU

Kuporomoka  kwa ufaulu katika shule za msingi na sekondari mkoani Dodoma, kumetafutiwa mwarobaini kwa kupeana mkakati wa kila kiongozi, mzazi, mwalimu na wanafunzi, kujituma na kuwajibika katika kuboresha elimu mkoani humo.
Wakichangia ripoti za wakuu wa wilaya na ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katika mkutano ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, wadau wa elimu zaidi ya 200 walisema, ufaulu utapatikana kama kila mmoja atawajibika kusaidia elimu.
Akielezea hali ya elimu katika Mkoa wa Dodoma, Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Maria Lyimo amesema, ufaulu umekuwa ukiongezeka japokuwa mkoa unashika nafasi za mwishoni kwa kushika nafasi ya 24 katika matokeo ya shule za msingi na nafasi ya 19 katika matokeo ya sekondari kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje (CCM) amesema, ufaulu utaongezeka kama watoto watapewa chakula shuleni na walimu watafundisha kwa bidii na wazazi watafuatilia maendeleo ya watoto.
Akiwasilisha taarifa ya utafiti uliofanywa katika shule mbalimbali mkoani Mhadhiri wa Udom, Dk Francis William alisema suluhisho la kufikisha maendeleo ya ufaulu wa elimu mkoani lazima wazazi wahamasike kuwahamasisha watoto kusoma.
Dk William alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwalazimisha watoto kuandika madudu ili wafeli waolewe au wafanye kazi za kulima au kuchunga mifugo.
Alisema mkoa ukiamua kufaulisha wanafunzi lazima kila kiongozi, Mkuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wote kuwajibika katika kufuatilia watoto wanafaulu masomo yao.
Akichangia mada hizo, Mwalimu wa Shule ya Mtakatifu Paulo Mjini Dodoma, Emmanuel Chisina alisema lazima kila mtendaji kuwajibika na wenyeji wasikae kando kusukuma vema maendeleo ya elimu mkoani.
Mzee Job Lusinde amesema, katika kuinua elimu kila mzazi, mwalimu na wadau wengine wanatikiwa kushiriki katika kampeni za kuinua elimu kila mti kwa nafasi na uwezo wake.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi alisema; “tusingoje serikali, kila mdau wa elimu anatakiwa kujiuliza ametoa mchango gani katika kupandisha ufaulu wa elimu mkoa huo.”
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Mahenge aliwaambia wakuu wa wilaya kuhakikisha wanatekeleza ahadi walizoweka katika kuinua elimu kwenye halmashauri zao na wajue wameweka kiapo cha kuinua elimu mkoani.

No comments

Powered by Blogger.