Heade

MIZIGO YA UGANDA KUPITIA TANZANIA KUONGEZEKA

Hatua ya Shirika la Reli la Uganda (URC), kuchukua tena udhibiti wa kuendesha na kukarabati reli zake, unatarajiwa kuwa chanzo cha kutengemaa kwa kipande cha reli, kilichokuwa hakipitiki kwa muda mrefu.
Kipande hicho ni kutoka Bandari ya Port Bell, Uganda hadi katikati ya jiji la Kampala, hivyo kufungua milango zaidi ya shehena ya nchi hiyo kupitia Tanzania. Kwa sasa shehena ya Uganda inayopitia Tanzania ni takriban 300,000 kwa mwaka, ikilinganishwa na mzigo wa nchi hiyo unaokwenda na kutoka nje ya nchi, ambao unafikia tani milioni saba kwa mwaka, ambapo sehemu kubwa kwa sasa inapitia Kenya.
URC imevunja mkataba na Kampuni ya Rift Valley Railways (RVR) yenye makao yake makuu Nairobi, Kenya, ambayo ilikuwa na dhamana ya kuendesha na kusimamia reli nchini Uganda. Kampuni hii imekuwa ikilalamikiwa utendaji wake, ikiwemo kushindwa kukarabati kipande hicho cha reli. RVR iliyokuwa inaendesha na kusimamia reli nchini Kenya, taarifa zinaonesha kwamba mkataba wake pia ulivunjwa nchini humo mwaka jana.
Tangazo la URC lililochapishwa katika gazeti la East African la Februari 3-9 mwaka huu, toleo namba 1214 linasema kwamba URC ilivunja mkataba na RVR tangu Januari 25 mwaka huu. Kuanzia tarehe hiyo, tangazo hilo linasema kwamba shughuli zote za usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na usimamizi wa miundombinu ya reli, itakuwa ni kazi ya URC na siyo RVR tena.
Akizungumza na Habari- Leo jana, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Janeth Ruzangi, alisema kwamba URC wakikarabati kipande hicho cha reli, itasaidia kuongeza shehena ya Uganda kupitia Tanzania na kwamba hiyo ni habari njema kwa wasafirishaji wa mizigo wa nchini Uganda na wasafirishaji wote wa mizigo nchini. Alifafanua kwamba kutokana na kipande hicho cha kilomita tisa cha reli kutopitika kwa muda mrefu, kulisababisha iwe vigumu kwa baadhi ya mizigo ya Uganda inayopitia Tanzania kusafirishwa, ikiwa katika mabehewa ya reli ambayo hubeba mizigo ya kontena.
“Mizigo inapokuwa haipo kwenye makontena inakuwa ghali kuisafirisha. Kwa hiyo kipande hicho kikikarabatiwa, mizigo mingi kwenye makontena itasafirishwa kwa reli hadi Mwanza na kuingizwa kwenye meli zinazobeba mabehewa kama MV Umoja na kisha kusafiri hadi bandari ya Port Bell, Uganda na kisha kwenda Kampala ikiwa kwenye mabehewa,” alisema Ruzangi.
Mwaka jana Serikali ya Uganda na Tanzania ziliingia katika makubaliano ya kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini, kwa lengo la kudumisha biashara kati ya nchi hizo mbili. Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (Marine Services Co. Ltd-MSL), Eric Hamissi, yenye makao yake makuu jijini Mwanza, alisema habari za Uganda kuvunja mkataba na RVR ni njema sana kwa Watanzania.
“Hiki kipande cha kilometa tisa kutoka Port Bell hadi Kampala tulikuwa tunakipigia kelele sana kwa sababu ndicho kilikuwa kinatunyima kiasi kikubwa cha mizigo ya Uganda kupitia Tanzania,” alisema kwa njia ya simu alipoongea na HabariLeo jana.
Alisema kwa sasa wanalazimika kusafirisha mizigo ya Uganda kupitia meli ya MV Umoja, ambayo imetengezwa kwa ajili ya kusafirisha mabehewa, lakini ikiwa haiko kwenye mabehewa kutokana na kipande hicho kutokamilika. “Serikali ya Uganda imetuita sisi kampuni yetu (MSL), TPA na Shirika la Reli kwenda kuangalia namna tutakavyoshughulikia usafiri wa Reli ya Kati hadi Uganda. Hii kwa kweli ni habari njema sana kwetu kwa sababu kipande hicho kikikamilika, mapato yataongezeka sana katika nchi yetu,” alisema Hamissi.

No comments

Powered by Blogger.