Heade

MAKAMU WA RAIS AWAHAKIKISHIA WANANCHI UPATIKANAJI WA DAWA ZA KUUWA WADUDU WAHARIBIFU WA PAMBA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Serikali itamaliza kabisa tatizo la uhaba wa dawa za kuuwa wadudu waharibifu wa zao la pamba.
Mhe. Makamu wa Rais ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Busega kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Lamadi wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Simiyu.
Amesema awamu ya kwanza ya dawa zimeshafika Simiyu kwa ajili ya kuwagawia wakulima wa pamba na akaahidi kuwa awamu ya pili ya kuleta dawa hizo inamalizika katika wiki iliyoanza jana tarehe 19/02/2018, hivyo tatizo hilo litakuwa limekwisha.
“Ninajua kuna kiasi kikubwa cha dawa kinakuja Simiyu dawa itakuwa nyingi na wakulima wote watapata, hatuwezi kuacha nguvu zenu zipotee bure na kwa kuwa Simiyu ni mkoa wa Viwanda na ndiyo unazalisha pamba kwa wingi tutajenga viwanda vinavyotumia pamba, kwa maana hiyo hatuwezi kuiacha pamba iharibike” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe.Makamu wa Rais wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Masanzakona baada kuweka  jiwe la msingi mradi wa maji wa Kiloleli amewahimiza wananchi kuchangia huduma za maji ili miradi ya maji iwe endelevu.
Alisema Serikali imedhamiria kumaliza kabisa tatizo la maji hapa nchini kwa kujenga miradi ya maji  hivyo ni vema wananchi wakaunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia huduma za maji ili kusaidia miradi hiyo kujiendesha. 
Akiwasilisha taarifa ya mradi wa Kiloleli kwa Makamu wa Rais, Mhandisi wa Maji Wilaya ya Busega, Mohammed Said alisema mradi huo utagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.6 mpaka kukamilika kwake mwezi Machi 2018  na utawahudumia wananchi wa vijiji vitatu vya Yitwimila B, Ihale na Ijitu.
 Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Busega, Mbunge wa Busega Mhe. Raphael Chegeni alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa wananchi wakati wa kampeni ya kuwapelekea mradi wa Maji wananchi wa kata ya Kiloleli.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameanza ziara ya kikazi ya siku nne(04) mkoani Simiyu, ambapo amepata fursa ya kuzungumza na wananchi pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Busega na Bariadi.

No comments

Powered by Blogger.