Heade

RAIS MAGUFULI AMLILIA KINGUNGE KUZIKWA JUMATATU DAR

Rais John Magufuli amesema, amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwiru.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyelitumikia Taifa kwa uzalendo na uadilifu, alifariki jana alfajiri katika hospitali ya taifa ya Muhimbili , anatarajiwa kuzikwa Februari 5, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Rais alisema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa chama cha TANU na baadaye CCM, na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya serikali.
“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu,” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Balozi Juma Mwapachu, alisema Kingunge atakumbukwa kwa mambo mengi kwani alikuwa ni kiongozi shupavu ambaye alifanya kazi kwa karibu na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Huu ni msiba wa Watanzania wote kwa sababu mzee huyu ni mwanasiasa mkongwe na mimi nikimfahamu toka mwaka 1967 katika siasa hizi alikuwa mpambanaji,” alisema Balozi Mwapachu. Kingunge alifariki jana alfajiri wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Victoria, Dar es Salaam mwezi mmoja uliopita.
Amefariki ikiwa ni mwezi mmoja tangu mkewe, Peras Ngombale Mwiru afariki dunia mwanzoni mwa mwezi uliopita, kutokana na ugonjwa wa kupooza. Kingunge aliruhusiwa kutoka hospitali na kwenda kushiriki maziko ya mkewe na kisha kurudi hospitali alikolazwa mpaka mauti yalipomkuta.
Mtoto wa marehemu Kingunge, Kinje Ngombale alisema ni majonzi makubwa kwa familia kuondokewa na wazazi wote wawili katika kipindi kifupi na kwamba huo ni msiba mkubwa. “Huu ni msiba mkubwa kwetu kama familia, lakini yote tunamshukuru Mungu, tumeupokea,” alisema Kije.
Alisema mzee wake baada ya kushambuliwa na mbwa, alipata maambukizi kwenye figo na ini yaliyodhoofisha afya yake na hatimaye kupoteza maisha wakati madaktari wakiendelea kupambana kuokoa maisha yake.
Kingunge-Ngombale Mwiru alikuwa kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini alitangaza kukihama Oktoba 4, 2015, na kuunga na rafiki yake, Edward Lowassa katika kusaka tiketi ya kuingia Ikulu kwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya Lowassa kuenguliwa katika mchakato ndani ya CCM.
Kaka wa marehemu Kingunge, Enock Ngombale alisema pengo hilo halitazibika kwani Kingunge alikuwa akitegemewa na familia kwa ushauri na mambo mbalimbali. Wakati huo huo, Chama cha siasa cha NCCR-Mageuzi, kimesema kimepokea kwa masikitiko kifo cha mkongwe huyo wa siasa nchini.
Katika taarifa yake kwa Habarileo jana, Naibu Katibu Mkuu wa NCCR_Mageuzi, Elizabeth Mhagama alisema: “Kwa masikitiko makubwa tunaungana na wanafamilia, marafiki, jamaa na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao katika maombolezo ya msiba huu… marehemu atakumbukwa sana kwa umahiri katika demokrasia ya vyama vingi nchini.”
Mzee Kingunge alikuwa kiongozi mwandamizi katika serikali za awamu zilizopita na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ikiwa ni pamoja na waziri katika wizara mbalimbali, ukuu wa mikoa na pia kwenye chama kama Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi CCM na nyadhifa nyingine. Alizaliwa Mei 30, 1932 mkoani Lindi.

No comments

Powered by Blogger.