Heade

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ASEMA HALI YA CHAKULA IMEIMARIKA

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema hali ya usalama wa chakula nchini imeimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula.
Aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma juzi wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11 lililoahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu. Waziri Mkuu alitaja mazao hayo kuwa ni pamoja na mahindi yaliyovunwa katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe na Rukwa.
“Matarajio yetu kuwa hali ya mavuno msimu huu itakuwa nzuri kwa sababu mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli ulikuwa wa kuridhisha katika maeneo mengi nchini,” alisema.


Alisema serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa hali ya utengamano na usalama wa chakula inaendelea kuwa imara kwa wananchi wote na kwa wakati wote. Waziri Mkuu alisema serikali inawezesha wafanyabiashara wa mazao ya chakula kuendelea kusafirisha na kuuza mazao ya chakula nje na ndani ya nchi na kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima waendelee kuzitumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao stahiki na kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa mavuno.

No comments

Powered by Blogger.