Heade

JAMII YA WATU WA TARIME WATAKIWA KUDUMISHA UMOJA KATIKA MASUALA YA KULETA MAENDELEO

Jamii ya watu wa Tarime imetakiwa kudumisha umoja na mshikamano katika masuala ya kuleta maendeleo ikiwa kama sehemu ya kuenzi muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ume endelea kuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa pande zote mbili.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 54 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 26 April kila mwaka Katibu wa Chama Cha Mapinduzi  CCM wilaya ya Tarime Bw. Mkaruka Kura amesema umoja na ushirikiano wa dhati katika juhudi za kuleta maendeleo ndio vitu muhimu vinavyoweza kuyabadilisha maisha ya watu.
“Waasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar hayati mwl. Julius Kambarage Nyerere na Abed Amani Karume wali elewa kuwa kuungana na kushirikiana katika mambo mbalimbali kutazifanya nchi hizi kuwa na nguvu na uwezo wa kujitengemea katika maamuzi jambo ambalo ni muhimu sana  katika mustakabali wa maendeleo, hivyo watu wa Tarime hawana budi kuweka kando tofauti zao za kisiasa, dini na kikabila kuhakikisha kwamba wanaungana na kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya wilaya ya Tarime na Taifa kwa ujumla”Alisema Mkaruka Kura.
Alisema, hadi sasa mataifa ambayo yamepiga hatua kubwa kiuchumi hususani yale ya bara la Ulaya yanaendelea kufanya juhudi za kuungana na kushirikiana katika mambo mbalimbali suala ambalo linayafanya yazidi kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kila uchao lakini jambo la kushangaza ni kwamba nchi nyingi zinazopatikana katika bara la Afrika haziko tayari kushirikiana.
“Kutokuwa tayari kuungana na kushirikiana kumesababisha kuchelewa kwa maendeleo kwa sehemu kubwa ambapo tatizo kubwa likiwa ni baadhi ya viongozi ndani ya Afrika kutokuwa tayari kushirikiana ambapo wengi wanahofia kupoteza nafasi za uongozi endapo watakubali kuweka umoja na mataifa mengine, kwani wengi wao wana uroho wa madaraka hupenda kuongoza muda wote na ndio maana hata wengine wana amua kubadilisha katiba ili kujilinda na kuendelea kusalia madarakani” Alisema Mkaruka.
Aidha, alisema Tanzania ni nchi pekee ambayo hubadilishana uongozi bila migogoro kwani rais akimaliza muda wake hupisha kufanyika kwa uchaguzi mwingine unao ruhusu mtu mwingine kuchaguliwa kuingoza nchi jambo ambalo mataifa mengi yameshindwa.

No comments

Powered by Blogger.