Home
/
NEW UPDATES
/
MENEJA WA TPA KORTINI KWA TUHUMA ZA UMILIKI WA MALI ZISIZOLINGANA NA KIPATO CHAKE
MENEJA WA TPA KORTINI KWA TUHUMA ZA UMILIKI WA MALI ZISIZOLINGANA NA KIPATO CHAKE
Meneja Uhasibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Prosper Kimaro, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka ya kuwa na mali zisizolingana na kipato chake.
Akisomewa mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo. Kimaro anadaiwa kumiliki nyumba 23, viwanja vitatu na magari saba vyote vikiwa na thamani ya Sh. bilioni 1.4.
Mawakili wa Serikali, Vitalis Peter akisaidiana na Lilian Wiliam, walidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2012 na 2016, wilayani Temeke, Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa mtumishi wa umma katika nafasi ya Meneja Uhasibu wa TPA, alikutwa na mali zisizoelezeka.
Mali hizo, kwa mujibu wa mawakili hao, ni nyumba mbili zilizoko mtaa wa Uwazi, Temeke zenye thamani ya Sh, 123,273,253 na nyumba moja iliyopo Yombo Vituka yenye thamani ya Sh. 12,956,000.
Peter alidai kuwa mshtakiwa alikutwa akimiliki nyumba 23 na viwanja vitatu vyote vikiwa na thamani ya Sh. 1,178,370,324.
"Mheshimiwa Hakimu mshtakiwa alikuwa na magari saba yakiwamo Toyota LandCruiser yenye namba za usajili T 395 DEJ lenye thamani ya Sh. 180,131,815, Mitsubishi yenye namba za usajili, T 506 CMT ya Sh. 38,464,861, Massey Ferguson yenye namba za usajili T 838 CHH ya Sh. 24,469,060.50, Trela lenye namba za usajili T 383 CNZ la Sh. milioni 4.5, Toyota Harrier yenye namba za usajili T 338 CVX ya Sh. 35,860,617.30, Trela lenye namba za usajili T 938 CVB la Sh. milioni 4.8 na Massey Ferguson yenye thamani ya Sh.19, 138,324.44." alidai Peter wakati akimsomea mashtaka kigogo huyo.
Alidai kuwa mali zote alizokutwa nazo mshtakiwa hazilingani na kipato chake cha zamani na cha sasa.Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.
Upande wa Jamhuti ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na haukuwa na pingamizi la dhamana.
Hakimu Simba alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamani wawili watakaowasilisha hati za mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni 200 kila mmoja na pia awasilishe hati zake za kusafiria mahakamani.
Hata hivyo, hadi Nipashe inaondoka mahakamani hapo, mshtakiwa alikuwa hajatimiza masharti ya dhamana. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Mei 3, mwaka huu.
No comments