MFANYABIASHARA ATIWA MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia mfanyabiashara wa samaki aliyefahamika kwa jina la Nicholas Light (25) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake kwa kumnyonga hadi kufa wilayani Nyamagana.
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi, Ahmed Msangi wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari hii leo Aprili 30, 2018 na kumtaja mwanamke anayedaiwa kuuliwa na mfanyabiashara huyo kuwa ni Victoria Swai (26) ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni inayohusika na masuala ya anga.
Kamanda Msangi amesema chanzo cha mauaji hayo inasemekana kuwa ni wivu wa kimapenzi ambapo inadaiwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa anamsaliti kimapenzi, jambo ambalo lilisababisha kuzua ugomvi kati yao na kupelekea Nicholas kumnyonga mwanamke huyo kwa kumkaba shingo akiwa ofisini kwake na baadae kukosa pumzi hadi kufariki dunia.
Aidha, Kamanda Msangi amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi na pindi uchunguzi utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu ili waweze kufanya mazishi.
Kwa upande mwingine, Kamanda Msangi amewapa pole ndugu na familia kwa msiba walioupata pamoja na kutoa wito kwa wakazi wa jiji la mkoa wa Mwanza hususani vijana kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi wanapokuwa kwenye migogoro.
No comments