Heade

RAIS MAGUFULI ALIVYOFUNGUA BARABARA YA LAMI YA IRINGA -MIGOLI-FUFU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua barabara ya lami ya Iringa – Migoli – Fufu yenye urefu wa kilometa 189 na ambayo inaunganisha Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Dodoma.

Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri (The Great North Road) imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 207.457 ikiwa ni ufadhili wa benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania imetoa asilimia 12.8.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kukamilika kwa barabara hiyo kumeondoa adha iliyowakumba wananchi kwa miaka mingi ambapo safari ya Iringa – Dodoma iliyochukua siku nzima ama siku kadhaa wakati wa mvua, sasa inachukua muda wa saa 2:30.

Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida na Mwakilishi wa AfDB Bw. Jeremy Aguma wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na taasisi zao, na wameahidi kukuza zaidi ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayosaidia kukuza uchumi wa wananchi kama inavyoelekezwa katika dira ya maendeleo ya mwaka 2025.

Wabunge wa Mkoa wa Iringa wakiongozwa na Mbunge wa Ismani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake zilizoyawezesha majimbo yao kupata miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, vituo vya afya na zahanati, Maji, uwanja wa ndege wa Nduli, Umeme, ruzuku ya elimu na dawa.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika ufunguzi wa barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kupata barabara ya uhakika na amewataka kuongeza juhudi katika uzalishaji mali hasa katika kilimo na biashara ili waweze kunufaika nayo.

Mhe. Rais Magufuli amezishukuru AfDB na JICA kwa kuendelea kuwa washirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania, na kwa namna ya pekee amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale kwa uchapakazi wake, ubunifu, uaminifu na uadilifu uliomwezesha kuiongoza TANROADS kwa mafanikio hasa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara na madaraja.

Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga barabara hiyo, Serikali inauboresha uwanja wa ndege wa Nduli ili uweze kupokea ndege kubwa zitakazoleta watalii wengi na wafanyabiashara katika mkoa wa Iringa na maeneo mengine ya kusini mwa Tanzania ili rasilimali zilizopo katika maeneo hayo ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ziwanufaishe wananchi kama wanavyonufaika wananchi wa Kaskazini mwa Tanzania.

“Ruaha ni hifadhi kubwa, nataka hifadhi hii iwe kitovu cha utalii, nataka nyinyi ndugu zangu wa Iringa mnufaike na utalii katika hifadhi hii kama wanavyonufaika kule kaskazini kupitia Serengeti, watalii wakija hapa wenye hoteli watapata wateja, wenye maziwa watauza, wenye matunda watauza, wenye mahindi watauza, mtapata hela” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Iringa kuwapuuza wanaodai Serikali inakopa sana, na kueleza kuwa fedha hizo hukopwa kwa masharti nafuu, riba ndogo na hulipwa kwa muda mrefu, na kwamba ndizo zinatumika kujenga miundombinu ya kuchochea uchumi.

Pamoja na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli sherehe hizo pia zimehudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wabunge kutoka kamati ya bajeti na kamati ya miundombinu, Maaskofu na viongozi wa vyama vya siasa.

No comments

Powered by Blogger.