Heade

MUNGU AKIWA NA MALENGO NA WEWE HAKUNA JAMBO BAYA LITAKALOKUSHINDA AU KUKUANGAMIZA




Mungu akiwa na mpango na mwanadamu, hata kama bado mtu hajatambua kuwa Mungu ana mpango juu ya maisha yake, hakuna jambo lolote baya litakalopangwa juu ya mtu huyo likamuweza.
Wakati mwingine huenda unajiuliza ilikuwaje hali mbaya uliyokuwa nayo katika kuugua kwako ambapo watu walikuacha wakakaa kando wakisubiri ufe lakini kwa hali ya kushangaza pamoja na vipimo vya matabibu kusema usingeweza kupona tena lakini ulitoka kwenye hali ya kufa na sasa wewe ni mzima unaendelea kuishi na ugonjwa uliokuwa unakutesa uliisha usahau na waliokuwa wakisubiri ufe wamerudi kukushuhudia.Nikuambie si kawaida !Mungu ana kusudi na wewe.
Pengine unajiuliza ilikuwaje nikapona katika ajali ile iliyokuwa mbaya kiasi kile kwa haraka unaweza usipate majibu, na huenda unaishi na swali hilo kwa muda mrefu bila majibu ,nikueleze kwamba mpango alio nao Mungu juu ya maisha yako ndio unayo yafanya hayo yote yasikuangamize ,usingekuwa unasubirishwa ili ulitimize kusudi la Mungu usingekuwepo leo.
Ukisoma katika Biblia takatifu kitabu cha Kutoka2:1-10 utaona habari za Musa, Musa alizaliwa katika kipindi kibaya sana kwa watoto wa kiume waliokuwa wanazaliwa wakati huo maana kipindi hicho mfalme wa Misri alikozaliwa Musa alikuwa ameamuru watoto wa kiume wote wanaozaliwa na wanawake wa kiebrania watupwe mtoni na wasiachwe kuishi hata kidogo.
Lakini kwa sababu Mungu alikuwa na mpango na Musa, mama yake  baada ya kumzaa alimwona kuwa ni mtoto mzuri na hakuwa tayari kumtupa kama walivyofanya wanawake wengine.
Hivyo akawaza sana jinsi ya kumnusuru na kifo akamficha kwa miezi mitatu na alipo ona hawezi kumficha tena, akatengeneza kisafina akamweka ndani yake kisha akaenda hadi mtoni akakiweka katika majani kando ya  mto.
Akamwacha hapo ,kumbe wakati huo huo binti Farao alikuwa akielekea mtoni kwenda kuoga na mara alipofika mtoni akakiona kisafina akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta, alipo kileta akaona ndani yake yumo mtoto analia  akasema bila shaka huyu atakuwa mtoto wa Waebrania akamchukua akamwangalia akampenda. 
Akasema nitamlea huyu awe mwanangu,pembeni alikuwepo umbu la Musa yaani dada yake Musa ,ambaye alikaa pembeni kusubiri kuona yatayo mpata mtoto , akamwuuliza binti Farao je? niende nikamwite mlezi katika wanawake wa kiebrania aje akunyonyeshee mtoto?, binti Farao akasema haya enenda kamwite, yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto.
Mama yake Musa alipofika pasipo kufahamika kuwa ni mama yake , binti Farao akamwambia mchukue mtoto huyu uninyonyeshee nitakuwa nakulipa mshahara na atakapokuwa mkubwa nitamchukua awe mwanangu. Hivyo Musa akaepuka kifo.
Watoto wengi wa kiume walitupwa mtoni na kupoteza maisha lakini unaona jinsi ambavyo Musa alinusurika kifo na hii ni kwa sababu Mungu alikuwa na mpango wa kuwaokoa wana wa Israel kutoka utumwani kupitia mkono ya Musa.
Mahali popote pale ulipo, haijalishi wewe ni mtu wa aina gani ,hali yako ya maisha, uwe mtu unayeishi maisha ya chini sana au vyovyote vile unavyoweza kuwa, Mungu akiwa na mpango na wewe hata  shetani ,adui zako wakuwinde na kukuwekea mitego hawatakuangamiza kamwe, mpango wa Mungu kwako lazima ukamilike. 
Hivyo ni vyema kutambua kuwa uhai ulio nao si bure ,kuishi kwako si bure usiogope kwa mambo unayoyapitia na usijione unaishi kwa bahati tu, kwa sababu ulipitia mambo magumu na mabaya ambayo wakati mwingine ukiyakumbuka yanakunyima amani na kuiondoa furaha yako tambua kwamba Mungu ana mpango na wewe.
Jamesmtiba@gmail.com

No comments

Powered by Blogger.