Heade

RAIS MAGUFULI ABAINI TATIZO KUBWA KWA WIZARA YA MAJI NA WIZARA YA ARDHI NA KUTOA MAAGIZO MAZITO

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli ameagiza wataalamu wote wa idara za maji katika halmashauri zote nchini kusimamiwa moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili kuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa na idara hiyo na kuwawajibisha wahusika pale miradi isipotekelezwa.

Rais Magufuli pia amewataka wataalamu wa ardhi na mipango miji katika halmashauri zote nchini kusimamiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa na idara hiyo na kuwawajibisha wahusika pale mradi unapotekelezwa visivyo.

Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo Mei 10, 2018 wakati alipokuwa anazungumza mara baada ya kumaliza zoezi la kumuapisha Mhe. Alphayo Japani Kidata kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na Bw. Msalika Robert Makungu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora na kusema hajaridhishwa na utendaji katika sekta maji na ardhi kutokana na usimamizi mbaya wa miradi mingi ya maji na usimamizi mbaya wa masuala ya ardhi na mipango miji.

"Sasa hivi kila mahali watu wanalalamikia maji, Wabunge wanalalamika, wananchi wanalalamika, serikali imetoa fedha lakini miradi haitoi maji, ukichunguza miradi hii inasimamiwa na wahandisi wa maji wa halmashauri ambao Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambaye ana wataalamu wa maji hana uwezo wa kuwawajibisha, wahandisi wanawajibika kwa madiwani, sasa hatuwezi kwenda kwa mtindo huo", amesema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli ameendelea kwa kusema "kwenye ardhi kuna matatizo mengi ya ardhi na mipango miji, watu wanadhulumiwa ardhi, ugawaji wa viwanja ni matatizo, maafisa ardhi  na mipango miji wanachelewesha vibali vya ujenzi, huku nako Katibu Mkuu wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi hana mamlaka ya kuwachukulia hatua, hili nalo tatizo".

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Magufuli amemtaka Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kukutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwele na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi kutengeneza muundo utakaozingatia maelekezo aliyoyatoa leo.

No comments

Powered by Blogger.