SERIKALI KUTUMIA SHILINGI BILIONI 131.47 KUTEKELEZA MIRADI YA KIMKAKATI
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, Serikali imezindua Mkakati wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye kuchochea upatikanaji wa mapato ili ziweze kujitegemea.
Mkakati huo umezinduliwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ambapo amesema kiasi cha shilingi bilioni 131.47 kitatumika kutoa ruzuku ya utekelezaji wa miradi 22 kwa halmashari 17 zilizoko katika mikoa 10 nchini, katika mwaka wa fedha 2018/19.
Ameitaja mikoa hiyo ambayo Halmashauri zake zimekidhi vigezo vya kunufaika na miradi ya kimkakati katika awamu ya kwanza ya mpango huo kuwa ni Dar es Salaam, Geita, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Morogoro, Mtwara, Pwani, Simiyu na Songwe.
Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Halmashuri zinajenga uwezo wa kujitegemea kwa takribani asilimia 80 hadi 100 ifikapo mwaka 2025, badala ya hali ya sasa ambapo halmashauri hizo zinategemea ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa zaidi ya asilimia 88.
Amezitaka halmashuri zitakazopata fedha za miradi hiyo kuhakikisha fedha hizo zinawekezwa kwenye miradi yenye tija, inayokuza ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya halmashauri.
Ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kubuni miradi ya kibiashara kwa ajili ya wananchi wanaowaongoza kwa kutengeneza ajira kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Alionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watendaji wanaosimamia miradi hiyo ikiwa watatumia fedha hizo kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa na kurejea kauli ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwamba kufuja fedha za Serikali katika kipindi hiki ni sawa na kunywa sumu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, amesema kuwa Serikali inazo fedha za kutosha kufanikisha mkakati huo na kutoa wito kwa viongozi wa Mikoa husika kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanisha miradi yenye tija ili ipatiwe fedha.
Alifafanua kuwa tayari Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika mkoa wa Dar es Salaam katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kujenga Kituo cha Mabasi cha Mbezi Luis, Ujenzi wa Soko la Mburahati katika Manispaa ya Ubungo, Ujenzi wa Soko la Kisasa la Magomeni katika Manispaa ya Kinondoni na Ujenzi wa Soko la Kisasa la Kisutu, Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya Vingunguti katika Manispaa ya Ilala.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI Selemani Jaffo (Mb) amesema kuwa Ofisi yake itaanza kufuatilia na kupima utendaji kazi wa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ili kuona kama wanaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliwapongeza Wakurugenzi walioonesha mfano katika kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kubuni miradi yenye tija na ya kimkakati iliyopewa Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango na kuwataka watendaji wengine waige mfano huo.
Baadhi ya miradi itakaotekelezwa na Halmashauri zilizokidhi vigezo ni pamoja na Ujenzi wa Masoko ya Kisasa, Ujenzi wa Maegesho ya Malori, Ujenzi wa stendi za kisasa, Maghala ya kuhifadhi mazao, Masoko ya Kisasa, Machinjio na Ujenzi wa Viwanda.
No comments