Heade

SERIKALI YAFUTA LESENI 11 ZA UCHIMBAJI MADINI


Tume ya Madini imefuta leseni 11 za uchimbaji madini na zimerudishwa serikalini bila hakikisho la wahusika kupewa tena.

Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Prof. Idris Kikula, alisema hatua hiyo imefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na kanuni ya 21 ya kanuni za madini (Haki Madini) na Tangazo la Serikali namba 1/2018.

Alibainisha kikao cha kwanza cha tume kilichofanyika mwishoni mwa Aprili, mwaka huu, kiliazimia kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 kwa lengo la kuhakikisha serikali inamiliki hisa zisizopungua 16 ya mtaji wa kampuni zinazomiliki mgodi wa kati na mikubwa na wazawa kushirikishwa ipasavyo.

“Pia kuwajulisha wamiliki wote wa leseni zote za kuhodhi maeneo kuwa leseni  zao zimefutwa kwa mujibu wa Sheria ya madini ya mwaka 2017 na zimerudishwa serikalini bila hakikisho la kupewa tena,”alisema.

Alisema waliopewa leseni hizo walikuwa wakisubiri mwenendo wa bei ya soko la madini duniani kupanda au kushuka. Alitolea mfano leseni ya urani iliyotolewa walikuwa wakiangalia bei ya soko la dunia litapanda lini.

“Kwa hiyo yale maeneo mamlaka ilikuwa haiingizi chochote. Ufutaji huo sio sisi Tume bali ni matakwa ya kisheria na zipo leseni zipo 11,” alieleza.

Alitaja orodha za kampuni ambazo leseni zake zimefutwa ni Kabanga Nickel Company Limited iliyokuwa na leseni namba RL 0001/2009, National Mineral Development Corporation Limited yenye leseni namba RL 0009/2009, Precious Metals Refinery Company Limited yenye leseni namba RL 0013/2014 na Bafex Tanzania Limited yenye leseni namba RL 0010/2014.

Zingine ni leseni namba RL 0011/2014 na RL 0012/2014 zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni ya Bafex Tanzania Limited, leseni namba RL0014/2014 ya kampuni ya Mabangu Mining Limited, leseni namba RL 0014 ya Resolute (Tanzania) Limited, Wigu Hill Mining Company Limited yenye namba RL 0016/2015 na Nachingwea Nickel Limited yenye namba RL 0017/2015.

Prof. Kikula alisema hadi Julai 4, mwaka jana, kulikuwa na maombi mapya ya leseni za uchimbaji wa kati zipatazo 15 na ya kuhuisha 21.

“Maombi ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini yalikuwa 4,345 katika ofisi za madini za mikoa na wilaya na hadi Julai 4, mwaka jana, kulikuwa na maombi 240 ya leseni za utafutaji wa madini,”alisema.

Alieleza kuwa kati ya maombi hayo, 86 yalishalipiwa ada ya kuandalia leseni na yaliyobaki hayajalipiwa.

“Waombaji wote wanatakiwa kukamilisha maombi yao ili yaendane na matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kama ilivyorekebishwa mwaka 2017,” alifafanua.

Kadhalika, Prof.Kikula aliyataja matakwa hayo ni waombaji kulipia ada za kuandalia leseni, kuwasilisha mpango mkakati wa namna ya kushiriki kwenye utoaji wa huduma za jamii kwa wakazi wanaozunguka mgodi pamoja na namna wazawa watakavyonufaika.

“Matakwa mengine ni waombaji wote wa leseni za utafutaji wa madini kuwasilisha cheti cha tathmini ya athari za mazingira, uthibitisho wa tathmini ya fidia na kutokuwepo kwa mgogoro katika eneo lililoombewa leseni ya uchimbaji madini,”alisema.

Alisema waombaji wote wa leseni baada ya kupata leseni na kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji wawasilishe mpango wa uhifadhi mazingira ambapo nyaraka zote zinazotakiwa zinapaswa kuwasilishwa kwa Mtendaji Mkuu wa Tume.

No comments

Powered by Blogger.