WAZIRI MAHIGA KUFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI ISRAEL
Waziri wa Mambo ya Nje, Augustine Mahiga atafanya ziara ya kikazi nchini Israel kuanzia kesho Mei 7, 2018 hadi Mei 10, 2018, ziara inayotokana na mwaliko wa Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Atakapowasili nchini humo, Dk Mahiga atafanya mazungumzo na Netanyahu na kushiriki uzinduzi wa ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Israel.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje iliyotolewa leo Mei 6, 2018 imesema Dk Mahiga anakuwa waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje kutoka Tanzania kufanya ziara nchini Israel.
Mbali ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, Waziri Mahiga atatumia ziara hiyo kuishawishi Serikali ya Israel iunge mkono juhudi za Serikali za kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.
Israel ni moja ya nchi zenye maendeleo makubwa katika sekta za kilimo, viwanda, uhifadhi wa maji, matibabu, ulinzi na usalama, mawasiliano na nishati ya joto ardhi.
“Kupitia ziara hiyo, ajenda ya uchumi wa viwanda ya Tanzania inaweza kupata ushirikiano mkubwa wa Israel kutokana na hatua kubwa ya kimaendeleo iliyofikia,” inasema taarifa ya wizara.
Kabla ya Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi Israel, ilikuwa inawakilishwa kupitia ubalozi wa Misri na ubalozi wa Israel nchini Kenya pia unawakilisha Tanzania hadi sasa.
Israel ni moja kati ya nchi sita ambazo Serikali ya Tanzania imefungua balozi mpya. Job Masima aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Israel.
No comments