WAZIRI UMMY MWALIMU APEWA TUZO YA HESHIMA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM), amepewa tuzo ya heshima na klabu ya soka ya Coastal Union ya jijini Tanga.
Coastal Union wametoa tuzo hiyo kwa Ummy, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake ambao ulifanikisha harakati zao za kurejea ligi kuu kuanzia msimu ujao baada ya kufanikiwa kuwa miongoni mwa timu sita zilizopanda msimu huu.
Tuzo hizo ambazo zimetolewa na baraza la wazee wa timu hiyo chini ya Mwenyekiti Salimu Bawaziri pia amekabidhiwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani pamoja na wadau wengine.
Ummy alijitolea kugharamia kambi za timu hiyo wakati wa michezo ya ligi daraja la kwanza pamoja na kulipa mishahara na posho za viongozi na wachezaji jambo ambalo liliongeza hamasa kwa wachezaji.
Coastal Union ni miongoni mwa timu sita zilizopnda ligi kuu msimu ujao. Nyingine ni Alliance Schools, Biashara Mara, KMC, African Lyon na JKT Tanzania ambazo zitachukua nafasi za Ndanda FC na Majimaji FC huku zingine zikiongeza idadi ya timu kutoka 16 hadi 20.
No comments