RAIS MAGUFULI ACHANGIA MILIONI 10 UJENZI WA MSIKITI MKUU JIJINI DAR ES SALAAM
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa dini kuwa wasemaji wa mambo yao na si kusemewa na wanasiasa.
Amesema hayo leo Juni 12, 2018 alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), unaojengwa Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Rais amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwa wasemaji wakuu wa mambo yao na si kuwaachia watu wengine ambao hawana uhusiano wowote na masuala ya kidini.
“Msiwe na wasemaji ambao si viongozi wa dini. Msiwatumie wanasiasa... mambo ya dini yazungumzwe na viongozi wa dini wenyewe,” amesema Rais Magufuli.
Amesema kuwapa uwanja wanasiasa kuwa wazungumzaji wa masuala ya kidini kunaweza kulitumbukiza Taifa katika hatari kwa kuwa wanasiasa wamekuwa na tabia ya kutaka kutumbukiza ajenda zao.
“Msitafute wasemaji kwa niaba ya maaskofu, mapadri, wachungaji, masheikh... kuweni wasemaji wa mambo yenu wenyewe. Mtakuwa mnatupoteza, Taifa mtalipeleka kubaya. Mambo yenu yasemeeni wenyewe kuwapa watu wengine mtawachanganya wasikilizaji,” amesema.
Rais Magufuli amemkabidhi Sh10 milioni kwa Mufti wa Tanzania, Abubakary Zubeiry zikiwa mchango wake katika kugharimia ununuzi wa saruji ili kuharikisha ujenzi wa msikiti huo unaotarajiwa kumalizika Aprili, 2019.
“Hela hii ikasaidie kununua mifuko 625 ya saruji ili msikiti huu ukamilike kwa wakati... nafahamu ujenzi wake unagharimiwa na Mfalme wa Morocco lakini nami nimeona nichangie sehemu hiyo ndogo,” amesema.
No comments