NJIA NZURI YA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO AU TATIZO KWA MCHA MUNGU
Katika maisha kuna changamoto mbalimbali na matatizo kadha wa kadha unayokutana nayo mtu wa Mungu, wewe ambaye umempa nafasi kubwa Mungu kuyaongoza maisha yako.
Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuyashughulikia matatizo na changamoto unazokutana nazo kwa njia sahihi ,nzuri na bora yenye uhakika wa kulimaliza tatizo lako.
Watu wengi wameshindwa kuyashughulikia na kuyatatua matatizo yao kwa kukosa njia nzuri ya kuyadhibiti na kuzishughulikia changamoto wanazokutana nazo na wengi hujikuta wanaongeza tatizo badala ya kulitatua tatizo.
Ni mara ngapi umekuwa mtu wa kurumbana, kurushiana maneno makali na hata kutoleana vitisho mathalani panapotokea mgogoro kati yako na mtu mwingine au kundi fulani.
Wakati mwingine umechukua maamuzi mabaya ambayo yanaleta madhara makubwa na kuongeza tatizo zaidi.
Ni muhimu sana kuelewa kuwa ukiwa mtu unaye mcha Mungu inakubidi hatua zako za kuyashughulikia matatizo ziwe za kipekee kwani wewe ni mwana wa mamlaka zilizo kuu ambazo hazishindwi na jambo lolote.
Ukisoma biblia katika kitabu cha Daniel 6:1-28 ,utaziona habari za Daniel ambaye watu walitafuta jinsi ya kumshitaki kwa Mfalme lengo lao likiwa ni kutaka kumharibia kazi na kuvuruga maisha yake kutokana na hila au wivu kwa sababu Daniel alionekana kuwa na sifa kuliko wakubwa na maliwali kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake.
Wakapanga kumkamata Daniel katika mambo ya sheria za Mungu wake hivyo wakapanga sheria iliyotaka mtu yeyote asimwabudu Mungu ndani ya siku thelathini isipokua waiabudu miungu ya mfalme na atakayekiuka atatupwa kwenye tundu la simba.
Mfalme akapokea na akaipitisha hiyo sheria kwa kuitia sahihi na kutangazwa kwa watu lakini Daniel hakukubali kuitii hiyo sheria bali alibaki kumtumainia Mungu.
Daniel 6:9-10;Basi Mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale,na ile marufuku.Hata Daniel alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu, akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali , akashukuru mbele za Mungu kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.
Mpenzi msomaji wangu unaona Daniel hakupingana na sheria hii kwa maneno au kutumia nguvu ya kimwili lakini alitulia akasema na Mungu na ukiendelea kusoma neno hilo utaona kuwa Daniel alitupwa kwenye tundu la simba lakini simba hakuweza kumwangamiza wala hakupatwa na dhara lolote, Daniel 6:16-23.
Daniel anapata ushindi kutokana na njia nzuri aliyo ichukua kushughulikia changamoto yake, Daniel aliamua kumtegemea Mungu na kumwomba kwa bidii ,asubuhi, mchana na jioni.
Je?ni mara ngapi umekumbwa na changamoto au tatizo lakini haukuchukua njia nzuri ya kuishughulikia changamoto yako kama mtu unaye mcha Mungu, ni muhimu sana kulikabili tatizo kwa njia inayompa Mungu nafasi kusimama na wewe, maana ndio njia pekee isiyoweza kushindwa na jambo lolote .
Ni matumaini yangu makubwa kuwa kwa maneno machache niliyokuandikia na vifungu vya biblia nilivyokukumbusha kuvisoma, yote hayo yatakufanya kuelewa zaidi umuhimu wa kulikabili tatizo au changamoto kwa njia ya kiungu na utakuwa mshindi kama Daniel kwa kila jambo baya litakalo pangwa kuya angamiza maisha yako.
Jamesmtiba@gmail.com
No comments