RAIS mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta (56) na Naibu Rais mteule,
William Ruto (50) wanatarajiwa kuapishwa leo, kuanza ngwe ya pili ya
uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua alisema Kenyatta ataapishwa
kwenye Kituo cha Kimataifa cha Michezo Moi, Kasarani jijini Nairobi,
kuanzia saa nne asubuhi. Leo ni siku ya mapumziko nchini Kenya.
Kiapo hicho kitaongozwa na Msajili Mkuu wa Mahakama, Anne Amadi na
kushuhudiwa na Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga. Sherehe hizo
zinazotarajiwa kuhudhuriwa na wageni 100,000 wa ndani na nje ya Kenya,
zitagharimu shilingi milioni 300 za Kenya (zaidi ya Sh bilioni 6.3 za
Tanzania).
Baada ya kiapo, jeshi litapiga mizinga 21 kumkaribisha Rais mpya.
Kenyatta amemwalika mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi uliopita,
kiongozi wa Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), Raila Odinga
ahudhurie sherehe hiyo.
“Wagombea wengine saba na wagombea wenza wao kwenye uchaguzi uliopita
wa Rais wamealikwa kwenye sherehe,” alisema Kinyua. Alitoa mwito kwa
wapinzani kusitisha mpango wa kumwapisha Odinga leo na badala yake
washirikiane na Serikali kwenye mambo yenye manufaa kwa Wakenya.
Kenyatta aliahidi kuwa Rais wa Wakenya wote, hata ambao hawakumpigia
kura Oktoba 26 na hatambagua au kumwadhibu yeyote kwa sababu za msimamo
wake wa kisiasa.
Alitaja vipaumbele vyake kuwa kwanza ni amani kwa Wakenya wote, na
pili kuhakikisha umoja wa Wakenya wote unakuwa msingi wa kupata
maendeleo wanayoyataka. Alitoa mwito kwa viongozi kuweka kando tofauti
zao za kisiasa na wafanye kazi pamoja kuboresha maisha ya Wakenya.
Juzi (Jumapili) Kenyatta alihudhuria ibada ya shukurani kwenye Kanisa
la Injili la Redeem Huruma, ambapo alisema sherehe za kuapishwa kwenye
Uwanja wa Kasarani, hazitakuwa kwa ajili yake kufurahia ushindi, ni za
Wakenya kusheherekea amani na umoja wao.
Alisema, kwa kuwa Kenya ni nchi ya kidemokrasia, ni kawaida
kushindania madaraka ya kisiasa, lakini ushindani huo usiwe kwenye
misingi ya ukabila au eneo anapotoka mtu, ila mawazo yatakayoboresha
maisha ya Wakenya.
“Kama ilivyo kwenye ushindani wowote, kuna washindi na walioshindwa,
lakini kwenye uchaguzi sisi wote ni washindi kama Wakenya. Baada ya
ushindani wa kisiasa wajibu wetu ni kuungana kuijenga nchi,” alisema
Kenyatta.
“Kwenye siasa ni kawaida kuwa na tofauti za kisiasa, lakini hilo
halimaanishi kwamba hatuwezi kuwa pamoja na kuishi pamoja kwa amani,”
alisema. Kwenye ibada hiyo, Kenyatta na Naibu wake, Ruto walipiga magoti
pamoja, wakawekewa mikono kichwani kuombewa.
Ruto alisema alikuwa kanisani hapo na Kenyatta kutekeleza ahadi yao
kwa Mungu kwamba kama angewapa ushindi watamtukuza. Alitoa mwito kwa
viongozi kuweka kando tofauti zao za kisiasa na wafanye kazi pamoja
kuboresha maisha ya Wakenya.
Msemaji wa Serikali ya Kenya, Erick Kiraithe alisema wakuu 20 wa
nchi, wamethibitisha kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Kenyatta, akiwemo
Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli ambaye ni kipenzi cha wengi ndani na
nje ya Afrika Mashariki.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu pia anatarajiwa kuwa
miongoni mwa watakaoshuhudia Kenyatta akiapa. Anatarajiwa kufika Kenya
leo asubuhi na ataondoka mara baada ya sherehe za kiapo.
Kenyatta na Ruto wanaapishwa kwa kuwa Novemba 20 mwaka huu, Mahakama
ya Juu nchini Kenya ilitoa hukumu kwamba ushindi wao kwenye uchaguzi wa
marudio Oktoba 26 ulikuwa halali.
Kenyatta na Ruto waligombea kupitia chama cha Jubilee kilichoanzishwa
Septemba 8 mwaka jana, kwa kuunganisha viongozi wakuu wa Muungano wa
Jubilee, The National Alliance (TNA), United Republican Party (URP), na
vyama vingine 10 vya siasa.
Kwa mara ya kwanza, Kenyatta na Ruto waliapishwa kuongoza Serikali ya
Awamu ya Nne baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Aprili 2013
kwenye kaunti zote 47 na diaspora. Uchaguzi mwingine utafanyika mwaka
2022 kupata viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa mujibu wa Kenyatta, Ruto atagombea urais. USHINDI WAKE Anaapishwa
kwa kuwa Novemba 20 mwaka huu, Mahakama ya Juu nchini Kenya,
iliidhinisha ushindi aliopata wakati wa uchaguzi wa Oktoba 26 mwaka huu.
Jaji Mkuu wa nchi hiyo, David Maraga alitangaza uamuzi huo wakati
akisoma hukumu ya majaji sita. Awali, Oktoba 30 mwaka huu Tume Huru ya
Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), ilimtangaza Kenyatta kuwa mshindi
kwa kupata asilimia 98.26 ya kura zilizopigwa.
Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alisema katika uchaguzi wa
marudio, Kenyatta alipata kura 7,483,895 kati ya kura halali 7,616,217
zilizopigwa kwenye majimbo 266 kati ya 291. Kwa mujibu wa Chebukati,
asilimia 38.84 ya Wakenya 19, 611,423 waliojiandikisha, walipiga kura
uchaguzi huo wa marudio.
Kura 37,713 ziliharibika. Awali IEBC ilimtangaza Kenyatta kuwa
mshindi wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8, lakini Septemba Mosi
Mahakama ya Juu Kenya ilibatilisha ushindi huo kwa maelezo kuwa taratibu
zilikiukwa.
Oktoba 26 mwaka huu, Wakenya walipiga kura na IEBC kupitia kwa
Chebukati ikatoa tangazo namba 10808 gazetini, kumtangaza Kenyatta na
mgombea mwenza wake, Ruto kuwa ni washindi.
Kulikuwa na wagombea wanane akiwemo kiongozi wa Muungano wa Vyama vya
Upinzani (NASA), Raila Odinga, Ekuru Aukot wa chama cha Third Way
Alliance, Cyrus Jirongo (United Democratic Party), Abduba Dida (Alliance
for Real Change), na wagombea binafsi Michael Wainaina, Joseph Nyaga na
Japheth Kavinga.
WASIFU WA KENYATTA Uhuru Kenyatta ni mtoto wa Baba wa Taifa wa Kenya,
Rais wa kwanza wa Jamhuri huru ya Watu wa Kenya, Jomo Kenyatta. Uhuru
alizaliwa Oktoba 26, 1961. Alisoma Shule ya Mtakatifu Maria jijini
Nairobi.
Baada ya hapo, alisoma sayansi ya siasa na uchumi kwenye Chuo cha
Amherst, Massachusetts nchini Marekani. Baada ya kuhitimu alirudi Kenya
akaanzisha kampuni iliyoitwa Wilham Kenya Limited, iliyonunua na kuuza
nje mazao ya kilimo.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Utalii Kenya na mwaka 2001 aliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Kenya, na
pia Rais Daniel Arap Moi akamteua kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.
Mwaka 2002 Kenyatta aligombea urais kupitia chama cha KANU, akabwagwa na
mgombea wa upinzani, Mwai Kibaki.
Baada ya uchaguzi huo alichaguliwa kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani
bungeni. Desemba mwaka 2007 Kenyatta alimuunga mkono Kibaki kwenye
uchaguzi wa Rais, na Januari mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Waziri wa
Serikali za Mitaa. Aprili mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu
na Waziri wa Biashara kwenye serikali ya mseto.
Tangu mwaka 2009 hadi 2012 mwanasiasa huyo alikuwa Waziri wa Fedha na
pia akaendelea na majukumu ya Naibu Waziri Mkuu. Kenyatta ana mke,
Margaret, walifunga ndoa mwaka 1989, na wana watoto watatu, Jomo
Kenyatta, Jaba Kenyatta na Ngina Kenyatta.
Wakati huo huo, Serikali ya Kenya imesema kuwa tayari wakuu wa nchi
11 za Afrika, wamethibitisha kushiriki katika sherehe za kuapishwa kwa
Kenyatta, huku nchi nyingine 13 zikitarajiwa kuwakilishwa ama na makamu
wao, mawaziri au ujumbe maalumu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, mbali ya
Netanyahu na Rais Magufuli, wengine waliothibitisha na nchi zao kwenye
mabano ni Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Ian Khama
(Botswana), Edgar Lungu (Zambia), Ismail Omar Guelleh (Djibouti), Hage
Geingob (Namibia), Faure Gnassingbe (Togo), Mohamed Farmajo (Somalia) na
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.
Nchi zitakazotuma wawakilishi na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni
Nigeria, Guinea, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Burundi
na Yemen. Senegal, China na Japan zitatuma ujumbe maalumu wakati Afrika
Kusini, Uingereza, Ukraine na India zitatuma mawaziri.
Wakati akiapishwa kuwa Rais wa Kenya kwa mara ya kwanza mwaka 2013,
wakuu wa nchi 12 walihudhuria. Katika hatua nyingine, Rais mteule wa
Kenya, Uhuru Kenyatta sasa anaitwa babu. Amepata mjukuu wa kike
aliyepewa jina Wanjiru.
Wanjiru ni jina la katikati la mke wa Kenyatta, Margaret. Mjukuu wa
mwanasiasa huyo alizaliwa juzi Jumapili kwenye Hospitali ya Aga Khan
jijini Nairobi. Kichanga Wanjiru ni cha mtoto wa kwanza wa Rais
Kenyatta, Jomo Kenyatta. Jomo ni jina la baba mzazi wa Rais Kenyatta
No comments