MSICHANA mwenye ulemavu wa ngozi (albino) amesema ushindi wake wa
kuwa namba moja kitaifa kwenye mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya
msingi nchini Kenya (KCPE) ni ushindi wa albino wote na kwamba, hakuna
anayeweza kutimiza ndoto zake bila alichoiita kuwa ni Ph.D yaani sala,
juhudi na nidhamu.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu Kenya, mtoto
huyo, Goldalyn Kakuya (14) amepata maksi 455 kati ya 500. Wanafunzi
993,718 walifanya mtihani huo. Mwaka jana mwanafunzi wa kwanza kitaifa
alipata maksi 437.
Mbunge wa Kuteuliwa, Dk David Sankok aliwapongeza wanafunzi sita
wenye ulemavu kwa kuwa miongoni mwa watahiniwa 100 bora kitaifa. “Leo
sitaki tusheherekee kwa ajili yangu tu, nataka tusheherekee ualbino,”
alisema Goldalyn.
Ijumaa iliyopita msichana huyo aliyekuwa akisoma kwenye Shule ya
Mtakatifu Anne Junior iliyopo Lubao kwenye jimbo la Kakamega, alikwenda
Ikulu ya Kenya kukutana na Rais Mteule, Uhuru Kenyatta na Naibu Rais
mteule, William Ruto.
Kenyatta na Ruto walimpongeza Goldalyn kwa mafanikio aliyopata.
Kenyatta aliahidi kumsaidia mtoto huyo atimize ndoto zake. Wakati akiwa
hapo Ikulu na wazazi wake, msichana huyo alipata fursa ya kuzungumza na
Rais Kenyatta na kumkumbatia kiongozi huyo.
“Nilimpongeza na nilizungumza na mwanafunzi bora wa mwaka huu KCPE
Goldalyn Kakuya. Goldalyn ana mwelekeo mzuri sana wa maisha yake ya
baadaye na utawala wetu utahakikisha kwamba anapata kila aina ya msaada
anaohitaji kutimiza ndoto zake,” alisema.
Katika hafla hiyo, wazazi wa msichana huyo walikabidhiwa hundi ya
Shilingi 100,000 za Kenya. Mama mzazi wa msichana huyo, Matilda Tanga,
alisema alifahamu binti yake angefanya vizuri kwenye mtihani huo, lakini
hakutarajia kuwa angekuwa wa kwanza kitaifa.
“Goldalyn ametuma ujumbe kwa watu wanaowadharau watoto wenye ulemavu
wa ngozi, na amethibitisha kwamba mtoto mwenye ualbino akipata upendo na
kupewa fursa wanaweza kuufikia uwezo wao,” alisema. Baba mzazi wa
Goldalyn, Harrison Tanga, anaikumbuka siku aliyozaliwa mtoto huyo,
Aprili 20, 2003.
“Nilipomwona (Goldalyn) nilimkumbatia mke wangu, Goldalyn ni dhahabu
yangu,” alisema Tanga. Wakati wa sherehe ya kumpongeza iliyoandaliwa na
Jumuiya ya Wenye Ualbino nchini Kenya, Goldalyn alisema alichofanyiwa ni
ujumbe kwa jamii kusheherekea ualbino na watu wenye ulemavu huo.
“Tunaweza kuwa vyovyote tunavyotaka,” alisema msichana huyo kwenye
sherehe hiyo katika ofisi za ASK, Nairobi. Alitoa mwito kwa wanafunzi
wenye ualbino kusoma kwa bidii. “Huwezi kutimiza ndoto zako bila PhD:
sala, juhudi na nidhamu,” alisema mtoto huyo.
Kwa mujibu wa Goldalyn, siku za nyuma alikuwa akikaa ndani tu ili
watu wasimwone, lakini akapata hali ya kujiamini na kwamba kwa sasa
hajisikii vibaya kuwa na ulemavu wa ngozi. Waziri wa Elimu, Dk. Fred
Matiang’i alitangaza matokeo siku 19 tu baada ya kumalizika kwa mtihani
huo, uliofanywa kuanzia Oktoba 31 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Mitihani Kenya (KNEC), matokeo
yamewahi kutolewa kwa sababu mchakato wa kusahihisha, uliharakishwa kwa
kutumia mashine ziitwazo automated Optical Mark Recognition Katika
matokeo hayo, wanafunzi 9,846 walifanikiwa kupata zaidi ya maksi 400.
Matiang’i alisema, watahiniwa wote kutoka shule za serikali na
binafsi, waliopata zaidi ya maksi 400 watapelekwa kusoma kwenye shule za
sekondari za serikali. Wanafunzi sita kutoka shule zenye mahitaji
maalumu, wamekuwa miongoni mwa watahiniwa 100 bora. Watahiniwa 2,360
walipata maksi chini ya 100.
Mchakato wa kuchagua watakaojiunga na kidato cha kwanza, unatarajiwa
kuanza Desemba nne na kazi ya kuwapangia shule itakuwa imekamilika
ifikapo Desemba 12. Matiang’i alifurahishwa na matokeo ya shule za
serikali. Alisema mwanafunzi wa pili kwa ubora kitaifa, ametoka shule ya
serikali ya bweni, Kathigiri na amepata maksi 447.
Alisema, mwanafunzi bora kutoka shule za wenye mahitaji maalumu
amepata maksi 426. Kwa ujumla, watahiniwa sita kutoka shule hizo
wamepata maksi zaidi ya 400. Kwa mujibu wa Matiang’i watahiniwa kwenye
mtihani huo, hawakufanya vizuri kwenye sayansi na masomo maalum.
Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimuagiza Waziri wa Elimu wa
nchi hiyo, Dk Fred Matiang’i wanafunzi ambao hakuwafanya mtihani KCPE
kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya kufiwa, ugonjwa au kujifungua,
wapewe wafanye.
Alitoa agizo hilo alipozungumza na Matiang’i kwenye ofisi za Kenyatta
katika jengo la Harambee kabla ya kutolewa kwa matokeo ya mtihani huo
Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Manoah Esipisu, alisema, katika mazungumzo ya
Rais Kenyatta na Dk Matiang’i, kiongozi huyo wa nchi alisema, wanafunzi
ambao hawakufanya mtihani huo kwa sababu zenye mantiki wakiwemo
waliokuwa wamefiwa na wazazi, waliojifungua na waliokuwa wagonjwa,
wapewe mtihani na kwamba, utaratibu kama huo unafanyika
No comments