MWANAMKE mmoja mkazi wa Mlodaa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma,
Monica Tupa (70) amesema amekuwa akizungushwa tangu alipofanyiwa kitendo
cha ubakaji Agosti mwaka huu na kuomba kusaidiwa ili haki iweze
kutendeka.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku 16 za kupinga
ukatili dhidi ya wanawake na watoto, alisema Agosti 14, 2017 alibakwa
majira ya usiku akiwa nyumbani wake. “Ilipofika asubuhi nikaongozana na
mjukuu wangu hadi kwa mkuu wa kitongoji kutoa taarifa, akaniambia nina
hela gani ya kuendesha kesi, ikabidi tuondoke kwenda ofisi ya mtendaji
tukakuta ofisi imefungwa,” alisema.
Alisema mtendaji hakuwepo kijijini lakini aliporudi alimpa barua ya
kwenda polisi kutoa taarifa wakati huo muda ulishakuwa umeshaenda sana.
Alisema baadaye mtuhumiwa alikamatwa na kupelekwa polisi.
“Nilipelekwa hospitali ya misheni ya Mvumi na waliponipima walinikuta
na dalili zote kuwa nimebakwa,” alisema. Alisema kama serikali inataka
kupunguza vitendo hivi ni muhimu kusaidia wananchi wa vijijini wasio na
uwezo wanapofanyiwa vitendo vya ukatili. “Nilibakwa nikaenda kutoa
taarifa lakini nikawa nazungushwa tu huku viongozi wengine wa kijiji
wakinikatisha tamaa kwa kunitolea maneno ya dharau,” alisema.
Kwa mujibu wa mratibu wa maadhimisho hayo Sarah Mwaga, mkoa wa Dodoma
ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha juu cha ukatili kuliko mikoa
mingine. Alisema kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa wa Tanzania
Demographic Health Survey (TDHS) wa mwaka 2010, mwanamke mmoja kati ya
watano au asilimia 20 wameshawahi kufanyiwa ukatili wa kindono maishani
mwao.
Pia asilimia 10 ya wanawake Tanzania walifanya vitendo vya kujamiiana
kwa mara ya kwanza kwa kulazimishwa na si kwa hiari yao. Alisema
asilimia 39 ya wanawake wote wameshawahi kufanyiwa ukatili wa kijinsia
wa kimwili ikiwemo kipigo, shambulio la mwili au kuumizwa mwilini katika
maisha yao.
No comments