JESHI la Polisi Zanzibar limeanza kufanya uchunguzi baada ya
kukamatwa kwa mfanyabiashara Naushad Mohamed Suleiman akiwa na kilo nane
za dhahabu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Kaimu Kamishna
wa Polisi Juma Yussuf Ali, alisema mfanyabiashara huyo aliyekuwa
mfadhili wa mashindano ya soka na timu ya Malindi Zanzibar, alikamatwa
baada ya jeshi hilo kupatiwa taarifa kuhusu kubeba almasi hiyo.
“Tumeanza uchunguzi ili kujiridhisha kama kweli mtuhumiwa anamiliki
almasi hizo au tuanze mchakato wa kumshtaki,” alisema Kamishna huyo na
kuongeza kuwa kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo ni jitihada za jeshi
hilo za kuhakikisha rasilimali za Tanzania zinalindwa.
Mtuhumiwa huyo alikuwa na kilo nane za dhahabu zenye thamani ya dola
za Marekani milioni 746.89 kulingana na bei ya sasa ya dhahabu, ambayo
ni dola za Marekani 41,564.45 kwa kilo pamoja na aina fedha za aina
mbalimbali kutoka nchi 15 duniani. Mfanyabiashara huyo alikuwa
anajiandaa kusafiri kwa ndege ya FlyDubai majira ya saa tatu usiku
akienda Dubai.
Rais John Magufuli hivi karibuni alianzisha hamasa ya kupambana na
ufisadi, rushwa na wizi wa kimataifa wa rasilimali za Tanzania. Agosti
31, mwaka huu, Mamlaka za Tanzania Bara zilikamata almasi zenye thamani
ya dola za Marekani milioni 15 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, zilizokuwa zikisafirishwa
kupelekwa Antwerp, Ubelgiji.
Almasi hizo zilikuwa zikisafirishwa kampuni ya uchimbaji madini ya
Williamson Diamonds, inayomilikiwa na raia wa Uingereza, Petra. Katika
muendelezo wa uchunguzi wa tukio hilo, maofisa wawili wa serikali
walishtakiwa kwa uhujumu uchumi.
Maofisa hao ambao ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Tathmini ya madini ya
almasi cha taifa, Archard Kalugendo na Mtathmini wa almasi kutoka Wizara
ya Nishati na Madini, walishtakiwa kwa kufanyia almasi hizo tathmini ya
na kusababisha serikali kupata hasara ya Dola za Marekani milioni 1.1
sawa na Sh bilioni 2.5.
Wakati huohuo, Kamishna huyo wa Polisi alibainisha kuwa kiwango cha
uhalifu ikiwemo mauaji visiwani Zanzibari, kimepungua kutoka mauaji ya
watu 34 mwaka jana hadi kufikia 24 mwaka huu.
Alisema mafanikio hayo yametokana na jeshi hilo, kuongeza ulinzi na
usalama katika maeneo mbalimbali visiwani humo. Aidha, alisema matukio
ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, pia yamepungua kutokana na
ushirikiano baina yao na serikali kuongezeka. Hata hivyo, alieleza kuwa
unyanyasaji wa majumbani na wizi katika makazi ya watu, kama vile mazao
ya shambani na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana bado ni matatizo,
ambayo polisi wanaendelea kuyafanyia kazi.
No comments