MATUKIO YA MAUAJI NA UBAKAJI YAPUNGUA MKOANI PWANI
Matukio ya mauaji mkoani Pwani mwaka huu yamepungua kutoka matukio 126 na kufikia matukio 34, ikiwa ni tofauti ya matukio 92 ya mwaka uliopita wa 2016.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Jonathan Shana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kwenye taarifa ya matukio yaliyotokea katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Januari 2016 hadi Desemba 2017.
Shana amesema kuwa matukio mengine ambayo yalitokea katika kipindi hicho ni pamoja na yale ya ubakaji ambayo nayo yamepungua katika kipindi hicho kutoka matukio 191 hadi matukio 21 ikiwa ni tofauti ya matukio 170.
“Matukio mengi yalikuwa ni yale ya uvunjaji ambapo kwa kipindi cha Januari 2016 hadi Desemba 2016 yalikuwa ni 771 lakini mwaka huu Januari hadi Desemba ni matukio 233 ikiwa ni upungufu wa matukio 538,” alisemaShana. Alisema kuwa matukio ya unyang’anyi wa kutumia nguvu yalikuwa 112 ambapo kwa mwaka huu yametokea matukio 43 huku mwaka huu yakiwa yametokea matukio 43 ikiwa ni upungufu wa matukio 69.
“Kwa upande wa matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2016 yalikuwa 31 mwaka huu ni manane, hali ambayo inaonesha matukio kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na utendaji wa kazi za polisi kwa kushirikiana na wananchi,” alisema Shana.
Aidha amesema katika kuelekea mwisho wa mwaka watahakikisha wanapunguza matukio ya uhalifu kwa kufanya doria za magari, pikipiki na miguu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili wananchi waweze kusherehekea kwa amani na utulivu. “Doria hizo zitakuwa za mtaa kwa mtaa nyumba kwa nyumba pamoja na kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo yale ya fukwe za bahari kama vile Bagamoyo hivyo watu wawe na amani katika kipindi hicho kuelekea mwaka mpya wa 2018,” alisema Shana.
No comments