Heade

WATUMISHI WA UMMA KIKAANGONI

Viongozi wa umma wamepewa siku tano kuanzia jana hadi Desemba 31, mwaka huu, wawe wamewasilisha tamko linaloonyesha mali zao, za wenza na watoto wao wenye umri usiozidi miaka 14 na ambao hawajaoa au kuolewa.
Imeelezwa kuwa kinyume cha hapo, kwa wale ambao watakuwa hawajafanya hivyo hadi ifikapo tarehe ya mwisho, hatua za kimaadili zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Tamko hilo linatakiwa kupelekwa katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kinyume cha hapo hatua zitakazochukuliwa kwa watakaokaidi agizo hilo ni pamoja na kupewa onyo, kushushwa cheo, kusimamishwa kazi, kufukuzwa kazi, kupelekwa mahakamani au mwenye mamlaka anaweza kutoa adhabu yoyote ile anayoona inafaa.
Kamishna wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Harold Nsekela alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Dar es Salaam.
Jaji Nsekela alisema kwa kuzingatia Kifungu cha 9 (1)(a) na (c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, viongozi wapya wanaochaguliwa au kuteuliwa wanatakiwa kujaza fomu hizo na kuzirejesha kwa Kamishna wa Maadili ndani ya siku 30 baada ya kupewa wadhifa.
Alisema pia kiongozi anapofikia mwisho wa kutumikia wadhifa wake, anatakiwa kujaza fomu za tamko la rasilimali na madeni na kuziwakilisha kwa kamishina. “Tunaomba viongozi wawasilishe hayo matamko kwa kuwa siku zilizobaki si nyingi. Hivyo basi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inawatangazia viongozi wote wa umma kwamba fomu za tamko la rasilimali na madeni zinapatikana kwenye tovuti yao ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz,” alisema Jaji Nsekela.
Alisisitiza kuwa, Sekretarieti hiyo inatoa mwito kwa viongozi wa umma ambao hadi sasa hawajapata fomu kutumia tovuti hiyo kuzipata kwa urahisi na kuzijaza. “Baada ya fomu hizo, kiongozi atatakiwa kuziwasilisha katika ofisi za Sekretari ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam, au katika ofisi zetu za Kanda ya Kati Dodoma, Kanda ya Ziwa Mwanza na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zilizoko mjini Mbeya.
“Kanda nyingine ni ya Kusini Mtwara, Kanda ya Magharibi Tabora, Kanda ya Kaskazini Arusha na Kanda ya Pwani, Kibaha kabla au ifikapo Desemba 31, mwaka huu,” alisema. Aliwakumbusha viongozi kuwa ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma kwa kiongozi kushindwa kutoa tamko bila sababu ya msingi.
Akielezea changamoto walizo nazo, alisema viongozi wengi sio waaminifu katika kutoa taarifa zao kwenye matamko. Jaji Nsekela alisema wanapaswa kuhudumia viongozi 16,169, lakini kutokana na uchache wa rasilimali fedha na watu, inabidi wahakiki watu wachache.

No comments

Powered by Blogger.