Heade

MIAKA 56 YA UHURU KUADHIMISHWA DODOMA TANZANIA IPO JUU

RAIS John Magufuli amesifi a mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana nchini katika kipindi cha miaka 56 tangu Tanzania Bara ilipopata Uhuru Desemba 9, 1961.

Akilihutubia Taifa kupitia wananchi waliofurika ndani na nje ya Uwanja wa Jamhuri, Makao Makuu ya Nchi, Dodoma jana, Rais John Magufuli alisifu mafanikio hayo akawaomba Watanzania wajivunie.

Rais Magufuli alisema Tanzania ni nchi pekee duniani yenye mfumo mzuri wa kurithishana mafanikio na kuyaendeleza kutoka kiongozi mmoja hadi mwingine, utaratibu ambao haupo katika nchi nyingi duniani.

Kutokana na mfumo huo, Rais Magufuli alisema anatamani siku moja aje aungane na wastaafu wengine kama Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal, Samuel Malecela na wengineo, akishuhudia maadhimisho hayo akiwa kama mstaafu.

“Nawapongeza waasisi na viongozi waliotanguliwa wa taifa hili kutokana na kuleta mafanikio nchini. Nchi nyingine kitu hiki ni kigumu kuona viongozi wakibadilisha madaraka kama inavyofanyika Tanzania,” alisema.

Akitoa historia ya Uhuru ulivyopatikana, Rais Magufuli alisema Tanzania ilitawaliwa na wakoloni kwa takribani miaka 76, kati yake Wajerumani walitawala kwa miaka 33 na Waingereza kwa miaka 43, lakini baada ya hapo nchi imepiga hatua kubwa na ya kujivunia.

Alisema harakati za kujikomboa zilianza na Tanu iliyoundwa Julai 7, 1954 na baadaye ikaunganishwa na ASP na kuunda CCM Februari 5, 1977, hiyo yote ilitokana na juhudi za waasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

Alisema katika kipindi hiki maendeleo makubwa yamepatikana mfano wakati nchi inapata Uhuru kulikuwa na barabara zenye urefu wa kilometa 33,600 na kati yake, barabara za kilometa 1,360, zilikuwa za lami, lakini leo barabara za lami ni kilometa 122,000, kati yake kilometa 12,000 tayari zimewekwa lami, 2,480 zipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi na 7,087 zipo kwenye maandalizi ya kujengwa kwa lami.

Rais Magufuli alisema kwa sasa nchini kuna madaraja 17 makubwa ambayo hayakuwapo wakati ule, vile vile kuna vituo vya afya 1,095 na hospitali zaidi ya 7,200 nchini. Alisema wakati nchi inapata Uhuru, kulikuwa na shule za msingi 3,100 hivi sasa kuna shule za msingi 17,379, huku shule za sekondari zilikuwapo zilikuwa 41 sasa zipo 4,817.

“Wakati huo kulikuwa na chuo kikuu kimoja sasa kuna vyuo vikuu 48, ambapo pia kulikuwa na madaktari 403 ambapo Watanzania walikuwa 12 sasa kuna madaktari 9,343 nchini,” alieleza.

Rais Magufuli alisema kulikuwa na wahandisi wawili, lakini hivi sasa wapo 19,164 waliosajiliwa sambamba na kulikuwa na makandarasi wawili na sasa wapo 9,350 waliosajiliwa. Alisema ukiachilia mbali kuongezeka kwa wastani wa miaka ya kuishi kutoka 37 hadi 61 kwa sasa, pia idadi ya Watanzania wakati huo ilikuwa kati ya milioni saba hadi tisa, lakini sasa kuna watu milioni 52.

Alisema mafanikio yaliyopatikana hata kama wale wengine hawapendi kusikia ni makubwa na yamepatikana katika sekta mbalimbali kuanzia kuanzia za maendeleo ya jamii hadi za ulinzi, hiyo yote imechangiwa na kutokana na nchi kulinda uhuru wake.

Rais Magufuli aliahidi kushirikiana kwa karibu na Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein katika kuhakikisha wanalinda mafanikio yaliyofikiwa na nchi mbili hizi katika kipindi hiki. Aliahidi kutekeleza ahadi zote walizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi, na kwamba yeye na Dk Shein watatimiza kwa weledi na kwa faida ya Watanzania wote bila kubagua na wataendelea kuwa watumishi wa Watanzania wote.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, Amri Jeshi Mkuu, Rais Magufuli mara alipoingia kwenye Uwanja wa Jamhuri alipigiwa mizinga 21 wakati ukiimbwa wimbo wa Taifa na wa Afrika Mashariki, alikagua gwaride lenye gadi 12 la majeshi ya ulinzi na usalama.

Pia aliona maonesho ya makomandoo, ndege za kijeshi, vikundi vya ngoma kutoka Kigoma, Songea na Zanzibar, kwaya kutoka Chunya na muziki wa Tanzania All Stars. Maadhimisho hayo pia yalipambwa na gwaride la wanafunzi, namna polisi wanavyoongoza misafara na hasa mazoezi ya namna ya kuokoa kiongozi wa juu ulifanywa kwa ushirikiano wa makomandoo, jeshi la anga la polisi, ulikuwa kivutio kikubwa.

Akitoa maoni yake kuhusu sherehe hizo, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Ibrahim Lipumba alipongeza mafanikio yaliyofikiwa, lakini alisema bado kuna mambo mengine ambayo serikali inatakiwa kutilia mkazo. Prof Lipumba alisema bado kuna tatizo la utapiamlo miongoni mwa watoto wengi, hivyo ni budi serikali kuendelea kufanya jitihada kuhakikisha jamii inanufaka na mafanikio hayo.

No comments

Powered by Blogger.