Mh rais John Pombe Magufuli amepigilia msumari kukamatwa kwa Mwenyekiti wa
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis
akidaiwa kutoa rushwa akisema atashangaa kama atachaguliwa mwenyekiti
anayewahonga fedha wamchague.
Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge alikamatwa jana na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dodoma. Alikamatwa kwa tuhuma
za kutoa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa umoja huo
akiwa nyumbani kwake maeneo ya mnada wa zamani wa Manispaa ya Dodoma.
Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Emma Kihanga alithibitisha kukamatwa
kwa Sadifa na kusema watatoa taarifa baadae kuhusu hilo. Kwenye mkutano
wa tisa wa UVCCM, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa
alisema kijana mpenda rushwa, mwizi, fisadi na tapeli ana mchango mdogo
kwa Taifa na hana tija.
“Ninavyozungumza hapa Mwenyekiti wenu yuko mahabusu kwa tuhuma za
rushwa, huo ndiyo umoja wa vijana?... lakini lazima niwaeleze, umoja wa
vijana tuliokuwa tunaujua na mimi nilikuwa mwanachama, siyo muelekeo
uliopo sasa.
“Umoja huu baada ya nchi kupata uhuru ilikuwa ni chachu ya kuwavuta
wananchi kujiunga na chama, ilikuwa sauti, mtete na chemchem ya fikra
mpya na chuo cha vijana kuandaliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi,”
alisema.
Rais Magufuli alisema pamoja na kwamba anajua vijana walifanya kazi
kubwa mpaka akaingia madarakani, lakini hakupelekewa orodha ya majina
kutoka UVCCM wakati akiteua viongozi katika ngazi mbalimbali.
Alisema anatambua vijana wa CCM ndiyo viongozi wa kesho, hivyo
alitumia mbinu zake mbadala kuwapata vijana aliowapa nafasi aliopata
wasifu wao kupitia njia mbalimbali. “Wengi walikosa nafasi kupitia umoja
wa vijana, nazungumza haya ili mpate nafasi ya kufanya mabadiliko Umoja
wa Vijana, msirudie makosa na mtambue jukumu lenu kwenye taifa hili na
kwa vijana wa vyama vyote,” alisema.
Alisema viongozi wa vijana wanaochaguliwa hapo ndiyo watakuwa
washauri wake. Alisema jumuia hiyo ina mali nyingi lakini zinatumika
ovyo na wamekuwa viongozi ambao wakati wa uchaguzi wanawekwa mifukoni na
wagombea.
“Mnakipeleka chama pabaya, mnatengeneza makundi ambayo hayatusaidii
kama nchi. Nawaomba mchague viongozi wanaofaa msije kuliangusha taifa,”
alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema UVCCM imekuwa kundi la kuwazuia watu wasiingie CCM kwa
kuwawekea vigingi watu wenye uwezo na mapenzi mema na chama. Rais
Magufuli alisema vijana walioamua kurudi CCM huko nyuma waliwahi
kunyimwa nafasi ya kujiunga na umoja huo hivyo wakaamua kuondoka lakini
sasa wameamua kurudi.
“Inawezekana wengine walijitahidi lakini wakakuta vizingiti,
ninawaomba msitengeneze vizingiti, umoja wa vijana uwe kimbilio la
vijana,” alisema. Alisema bado ana imani kubwa na vijana na wengi ambao
amewachagua kushika nafasi mbalimbali za uongozi hawajamuangusha.
Alisema ndani ya chama hicho sasa anahitaji vijana wanaochukia
ufisadi, wanaoweza kutetea nchi, ambao hawataweza kununuliwa na mtu.
Aliwataka vijana kuchagua viongozi ambao siyo wala rushwa na siyo kwa
kufuata ukabila bali wachague viongozi madhubuti wanaotanguliza maslahi
ya taifa mbele kwani chama hicho ni chama kinachojitambua chenye maadili
mema.
Aliwataka vijana kujitambua kwani wakati wa kushika dola ni sasa
lakini asingependa kuacha nchi kwa viongozi wala rushwa kwani itakuwa ni
usaliti kwa nchi na waasisi wa nchi hii, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere
na Mzee Karume.
“Mimi ni Rais lakini siyo Rais wa maisha yote, nafasi hizi za uongozi
ni zetu vijana lakini tusingependa tunapoondoka tunamuachia kijana mla
rushwa,” Rais Magufuli aliwaambia vijana. Alisema anawatambua vijana
wenye uwezo ndani ya chama hicho na atahakikisha anatoa nafasi za
uongozi kwa vijana ambao wana uwezo na utaalamu mbalimbali ndani ya
chama hicho.
Aliwataka pia vijana kuendelea kujibu hoja mbalimbali zinazoandikwa
na watu kwenye mitandao ya kijamii kwa upotoshaji. Kuhusu mali za UVCCM,
Rais Magufuli alisema mali za umoja huo zimekuwa zikitumika ovyo
ikiwemo viwanja na majengo na akawataka watakaochaguliwa wasibweteke
bali waanzishe miradi na kwamba haoni kama kuna ugumu wa kuwa na miradi
mikubwa.
“Kigugumizi kilikuwepo utampa nani huu mradi utapona? kama jengo la
umoja wa vijana la Dar es Salaam haijulikani kiasi gani kinaingia kila
mwaka, kuna wengine wamekabidhiwa vyumba vyao, kuna petrol station
Songea hawajui fedha zinaingia kwa nani,” alisema Rais Magufuli.
“Mmekuwa na viongozi ikifika wakati wa uchaguzi wamekuwa wakiwekwa
mfukoni na wagombea, tunakipeleka chama pabaya tunatengeneza magumu
ambayo hayatusaidii nchi hii, naomba vijana chagueni kwa kufikiria A-Z
ili msije kuliangusha Taifa,” alisema kuhusu viongozi UVCCM kuwekwa
mfukoni.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid
Mtulia alisisitiza kuwa kuhamia kwake CCM ilikuwa ni uamuzi wake binafsi
na siyo kwamba amenunuliwa na Rais Magufuli kama watu wanavyoeneza.
Alikiasa chama kujiandaa kwa uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo
mbalimbali hasa Kinondoni, Dar-es-Salaam ili jimbo hilo liende CCM na
kuongeza idadi ya majimbo wanayomiliki kutoka manne na kuwa matano.
Aliyekuwa mbunge wa Kigoma kusini (NCCR), David Kafulila alisema
sababu kubwa ya kujiunga CCM ni uwepo wa Utu na Usawa ndani ya chama
hicho na ajenda ya ufisadi aliyokuwa anaipigania wakati akiwa upinzani
kuhama na kubebwa na kutekelezwa na CCM.
Aliyewahi kuwa mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali alisema ameamua
kujiunga na CCM ili kujiunga na timu ya ushindi. “Zimepigwa propaganda
nyingi, Rais utasemwa maneno mengi kuwa unawanunua wapinzani, huo ni
udhaifu na wanaosema hivyo ni wadhaifu na tusiruhusu watu wachache
kutumia propaganda za kudhuru taifa letu,” alisema.
No comments