Heade

MUHIMBILI YAPUNGUZA GHARAMA

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita (2015 -2017), ikiwamo kuanzisha huduma mbalimbali, kuboresha zilizokuwepo na pia kuwekeza kwenye nguvu kazi.

Hiyo ni pamoja na kuanzisha huduma ambazo zilikuwa zikipatikana nje ya nchi pekee, ambako imefanikiwa kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi na kusimamia makusanyo ya mapato.

Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha hospitali hiyo, Aminieli Eligaeshi alisema katika kipindi cha miaka miwili, MNH imeanzisha huduma ya kupandikiza vifaa vya usikivu, iliyoanzishwa Juni mwaka huu, ambayo jumla ya watoto 6 walipata huduma hiyo kwa mara ya kwanza nchini.

Nyingine ni kukarabati jengo la zamani lililokuwa linatumika kwa shughuli za ofisi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kuongeza wadi 3 za kulaza wajawazito zenye vitanda 91.

Pia upanuzi na ukarabati wa Jengo Kuu la Upasuaji ambao umeongeza huduma za upasuaji kutoka watu 11,576 katika mwaka 2014/15 hadi kufikia watu 17,167 katika mwaka 2016/17.

“Hili ni ongezeko la asilimia 48.3 na haya ni mafanikio makubwa kwa taasisi yetu,” alisema Eligaeshi na kuongeza kuwa nyingine ni kukarabati wadi mbili na kuifanya wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kuwa yenye vitanda 18.

Aidha, Muhimbili imekarabati wadi 35 na kuifanya kuwa ICU ya kina mama yenye vitanda 10, pia imekarabati wadi namba 37 na kuifanya ICU ya watoto wachanga yenye jumla ya vitanda 21 na vitanda 6 vya “kangaroo mother.” Jumla ya vitanda vya ICU vimeongezeka kutoka 6 hadi kufikia 76.

“Hospitali pia imefunga mifumo ya ‘medical gas’ katika ICU zote na ‘recovery room’ ya jengo kuu la upasuaji,” alifafanua msemaji wa Muhimbili. Alisema Muhimbili imekarabati jengo la upasuaji la wajawazito na kukarabati jengo la upasuaji watoto wadogo, ambao awali walikuwa wakifanyiwa upasuaji watoto 15 hadi 20 sasa wanafanyiwa 40.

“Pia tumefanya ukarabati jengo la upasuaji wa kinywa na ukarabati wadi namba 18 ambayo kwa sasa inatumika kulaza wagonjwa wa kulipia yenye vitanda13,” alisema. Aidha, alisema katika miaka hiyo miwili hospitali hiyo kuu nchini, imekarabati jengo la Huduma za Dharura, kufufua mashine ya MRI na kufunga mashine ya kisasa ya CT-Scan na kununua mashine kubwa mbili za kusafisha vifaa.

Mbali na hayo, imefunga mitambo kwa ajili ya kuanza huduma za tiba mtandao (telemedicine) kwa lengo la kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo na pia kuwajengea uwezo madaktari katika hospitali za chini.

“Daktari anaweza kumuona mgonjwa kisha kwa njia ya mtandao akatuma huku vipimo vya mgonjwa daktari akaangalia na kumwambia matibabu yake, hii itapunguza idadi ya wagonjwa wanaokuja Muhimbili na kujenga uwezo wa madaktari wa huko chini,” alieleza Eligaeshi.

Alisema Muhimbili pia imenunua vifaa muhimu vya ICU na imeongeza juhudi za ukusanyaji wa damu na kufikia kiwango cha asilimia 79 ya mahitaji ya hospitali wakati awali ilikuwa chini ya asilimia 50.

“Katika kipindi hicho, pia tumepeleka wataalamu 37 nje ya nchi kwa ajili ya kupata mafunzo ya huduma za usingizi,” alisema Eligaeshi. Mafanikio mengine ni upandikizaji figo na vifaa vya usikivu na kuendelea kudhamini wafanyakazi wanaosoma katika vyuo vikuu vya afya nchini na nje; kuingia Mkataba na Serikali ya Cuba na kupata wataalamu wa afya 16 kutoka Cuba ambao watashiriki katika kutoa huduma na kutoa ujuzi kwa wataalamu wa Kitanzania.

Kuhusu mapato, msemaji huyo alisema fedha za Mfuko wa Dawa zimeongezeka na kufikia Sh bilioni 1.5 na kuwezesha upatikanaji wa dawa kufikia asilimia 95. Pia imeongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka wastani wa Sh bilioni 2 kwa mwezi na kufikia Sh bilioni 4.2, huku ikiongeza viwango vya motisha kwa wafanyakazi.

Katika huduma ya matibabu ya figo, mbali ya kuanzisha huduma ya upandikizaji figo, imepanua eneo la kusafisha figo na kuongeza vitanda 27 zaidi hadi kufikia jumla ya vitanda 44 vya kusafishia figo. “Huduma za kusafisha figo zilitolewa mara 12,370 ukilinganisha na mara 7,549 katika mwaka 2014/15,” alisema.

Katika miaka hiyo miwili, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilisimamia maboresho ya Idara ya Magonjwa ya Moyo ambayo kwa sasa imekuwa taasisi kamili inayojitegemea ambayo sasa ni Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

No comments

Powered by Blogger.