Muungano wa upinzani nchini
Kenya NASA, umetangaza kusitisha shughuli ya kumuapisha kiongozi wa
muungano huo Raila Odinga na kusema kwamba shughuli hiyo imeahirishwa
kwa tarehe nyingne ambayo haikutajwa.
Raila Odinga ambaye anaendelea
kupinga kuchaguliwa kwa rais Kenyatta na Stephen Kalonzo Musyoka,
walikua wanatarajiwa kuapishwa siku ya Jumanne Desemba 12 kama rais na
makamu wa rais mtawalia wa Jamhuri ya Kenya.
Wajumbe kutoka nchi za magharibi na Kanisa wanapendelea mazungumzo
kati ya rais Kenyatta na Odinga yafanyike kufuatia wasiwasi kuwa njia
iliyochaguliwa na upinzani ilikuwa inalenga kuzusha machafuko.
Siku ya Jumamosi rais Kenyatta alisema hayuko tayari kwa mazungumzo yoyote kuhusu mabadiliko ya uchaguzi.
Vyombo vya usalama vimejiandaa kuhakikisha haviruhusu mkusanyiko wa
upinzani siku ya Jumanne jijini Nairobi wakati rais Uhuru Kenyatta
atakuwa akiwaongoza wakenya kuadhimisha siku kuu ya Jamhuri katika
uwanja wa Kasarani.
Shinikizo zimekua zikiongezeka kumtaka kiongozi wa muungano wa
uypinzani nchini Kenya kuachana na mpango wake wa kuapishwa kama rais wa
watu siku ya Jumanne Desemba 12.
Katika taarifa iliyotolewa leo na muungano wa NASA ni kuwa tarehe
mpya ya kuapishwa kwa Bw. Odinga na Musyoka, na pia kuzinduliwa kwa
mabunge ya wananchi itatangazwa baadaye.
Odinga alijiondoa kwenye uchaguzi mkuu ambao ulifanyika tarehe 26 mwezi Oktoba ambapo Uhuru Kenyatta aliibuka mshindi.
Uchaguzi huo wa tarehe 26 ulikuwa ni marudio ya uchaguzi mkuu, baada
ya mahakama ya juu nchini nchini Kenya kufuta matokeo ya uchaguzi wa
Agosti 8 mwaka 2017.
No comments