Mkoa wa Njombe umetajwa kuongoza kuwa na asilimia 11.4 ya
watu wanaishi na virusi vya Ukimwi huku Zanzibar wanaoishi na virusi
hivyo ni chini ya asilimia 1.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa
ametoa takwimu hizo leo Desemba 1 katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi
Duniani ambayo Kitaifa imefanyika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Dk Chuwa amesema mkoa wa Lindi umekuwa wa mwisho kwa watu wenye virusi
vya ukimwi na idadi ya asilimia 0.1 huku maambukizo kwa Jiji la Dar es
Salaam yamepungua hadi kufikia asilimia 4.7 ikiwa na maana watu 133,971
wanaishi na ugonjwa huo.
Mkurugenzi huyo amesema kwa ujumla watu 1.4 milioni nchini Tanzania
wanaishi na virusi vya Ukimwi na takwimu hizo ndiyo rasmi hivyo asitokee
mtu au kikundi cha watu kupotosha.
"Nasema kwa sababu kuna watu wanakurupuka na kuja na takwimu zao. Naomba
watambue takwimu ni fani kama fani nyingine na zina miiko yake,"
amesema Dk Chuwa
Hata hivyo, Dk Chuwa amesema Serikali haimzuii mtu au kikundi kufanya
utafiti ila ni lazima awasiliane na ofisi ya takwimu wapitie dodoso zake
kabla ya kuruhusiwa kufanya.
Amesema atakayekiuka na kupotosha takwimu adhabu yake iliyowekwa
kisheria ni kifungo cha miaka mitatu au faini Sh10 milioni au vyote kwa
pamoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na virusi vya
Ukimwi, Justin Mwinuka ameiomba Serikali kutengeneza Sheria
zitakazoratibu upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya ukimwi (ARV).
Mwinuka amesema uwepo wa sheria hiyo utasaidia kuwabana watu wanaofanya
biashara kupitia dawa hizo.Amesema wagonjwa wengi hawapati dawa kutokana
na kushindwa kumudu gharama.
"Tuna changamoto ya uhaba wa dawa na zinazopatikana zinauzwa sasa wagonjwa wanashindwa kupata fedha za kununua,"
Mwinuka pia ameomba watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kuingizwa kwenye
mpango wa kaya maskini Tasaf ili waweze kutatua changamoto ya uhakika
wa lishe.
No comments