MTOTO wa miaka saba aliyelelewa kama mtoto wa kike kutokana na
maumbile yake kutoeleweka vema, baada ya vipimo vyote katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH), ameonekana kuwa ni mwanamume, hivyo amefanyiwa
upasuaji wa kwanza wa kushusha kokwa (mbegu za kiume) kwenda kwenye
korodani ili kumrejesha katika hali ya kawaida.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH, Zaitun Bokhary alisema hayo
alipofanya mahojiano maalumu na HabariLeo kuhusu kambi ya wiki moja
iliyowekwa kwa ajili ya kufanya upasuaji ambao ni mgumu, wakishirikiana
na wataalamu watano kutoka Chuo Kikuu cha Oxford nchini Marekani.
Dk Bokhary alisema upasuaji huo ni hatua ya kwanza katika kumrejesha
mtoto huyo katika hali ya kawaida, hatua nyingine za upasuaji zitafuata,
kwani atafanyiwa upasuaji kwa hatua tatu.
Alisema kwa kuwa mtoto huyo vipimo vimeshaonesha kuwa ni wa kiume,
wametoa ushauri kwa wazazi wake hususan baba yake kuwa karibu na mtoto
huyo ili kumfanya asijisikie vibaya, kwani awali alikuwa akijisaidia
haja ndogo kama mtoto wa kike, pia alikuwa amepewa jina la kike ikiwa ni
pamoja na kuvaa nguo za kike.
“Tumemshauri baba yake kutembea mara kwa mara na mtoto wake, pia
kwenda naye katika michezo ya kiume, ikiwa ni pamoja na kuanza
kumvalisha mavazi ya kiume. “Mtoto huyu alipoanza kuvaa nguo za kiume
kwa mara ya kwanza alikuwa akijisikia aibu kwa kuwa alishazoezwa mambo
ya kike, lakini tunaendelea kutoa ushauri kwa wazazi ili wawe karibu na
mtoto wao asijisikie tofauti yoyote,” alisema daktari huyo.
Aliongeza kuwa kwa kuwa tayari mtoto huyo alikuwa akisoma katika
shule ya msingi mojawapo jijini Dar es Salaam, hospitali hiyo inafanya
utaratibu kupitia kwa daktari wake ili kuandika barua kwa Wakala wa
Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita), atambuliwe kama mwanamume, ikiwa ni
pamoja na kuhamishwa shule aliyokuwa akisoma.
Alisema kuwa na sasa mtoto huyo, amehamishwa nyumbani kwao anakaa na
ndugu zake eneo lingine ili aanze kuzoea mazingira mapya ya maumbile
yake. Pia Dk Zaitun alielezea upasuaji mwingine mgumu uliofanyika ni wa
mtoto wa siku mbili ambaye alikuwa na tatizo katika mfumo wa nyongo,
njia ilikuwa imefungwa ilibidi apasuliwe kufungua njia ili mfumo wa
nyongo uendelee kama kawaida.
“Kwenye mfuko wa nyongo kulikuwa kumetengeneza uvimbe nyongo isipite
vizuri, hivi sasa baada ya upasuaji anaendelea vizuri,” alisema. Daktari
bingwa huyo wa upasuaji wa watoto, alieleza upasuaji mwingine
walioufanya ni kwa mtoto aliyekuwa na saratani ya figo zote mbili, moja
ilitolewa na nyingine ilikuwa haijalika ikaondolewa sehemu ya tatizo
bila kuathiri mfumo wa misuli.
Alisema upasuaji wote huo umekwenda vizuri, hali za watoto hao
zinaendelea vema. Alisema kambi ya upasuaji huo ilikuwa Novemba 27 hadi
Desemba Mosi, mwaka huu iliongozwa na Daktari Bingwa Mshauri Mwelekezi
wa Upasuaji wa Watoto, Profesa Kokila Lakhoo kutoka Chuo Kikuu hicho cha
Oxford. Alisema Dk Lakhoo amekuwa akija hospitalini hapo kila mwaka,
kusaidia ule upasuaji ambao ni mgumu, na huu ni mwaka wake wa tano
kufika nchini
No comments