MCHUNGAJI na waumini wa Kanisa la The Evangelistic Assemblies of God
(EAGT) mtaa wa Eden 'A' Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa, wamekesha
wakimuombea marehemu wao afufuke, wakidai alikufa kwa nguvu ya giza.
Elizabeth Lwitiko (30) alifariki dunia juzi saa tatu asubuhi kutokana
na matatizo ya uzazi, wakati akijifungua pacha, aliowaacha hai na
wametafutiwa mlezi.. Mchungaji Jacob Lwitiko aliongoza waumini wake,
kuchukua mwili wa marehemu chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga na kuiweka kwenye madhabahu ya kanisa
hilo na kufanya maombezi, wakiamini kuwa huenda atafufuka.
Mchungaji Lwitiko ni kaka wa Elizabeth na aliachiwa uongozi wa kanisa
hilo na kaka yake, Amos Lwitiko, mwanzilishi na kwa sasa yuko Makambako
mkoani Njombe. Mwenyekiti wa Mtaa wa Edeni “A” lililopo kanisa hilo,
Gerald Mwazembe alikiri kuwepo kwa mkasa huo, uliowashitua wakazi wa
jirani kwani ni mara ya kwanza kutokea.
Akisimulia, alisema kuwa Elizabeth alifariki dunia saa tatu asubuhi
katika Kituo cha Afya cha Mazwi mjini hapa kutokana na matatizo ya
uzazi, ambapo alipungukiwa damu mwilini baada ya kujifungua salama kwa
njia ya kawaida watoto pacha ambao wako hai.
“Mwili wa marehemu ulihifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, lakini waombolezaji na mchungaji wa kanisa
hilo waliuchukua mwili huo wakiamini alikufa kishirikina na kwamba
wakimwombea angeweza kufufuka,” alieleza.
Alisema mwili ulipofikishwa kanisani hapo, uliwekwa madhabahuni na
ibada ya maombezi iliyoambatana na nyimbo na midundo ya ngoma,
ilifanyika kuanzia saa sita mchana hadi usiku wa manane huku milango
ikiwa imefungwa, wakiamini kuwa atafufuka.
“Ilipofika usiku wa manane niliwapigia simu Polisi ambapo askari wa
kikosi cha doria walifika kanisani hapo, baada ya mazungumzo marefu
waliagiza mwili wa marehemu urejeshwe na kuhifadhiwa kwenye chumba cha
kuhifadhia maiti ili usiharibike,” alieleza.
Aliongeza Polisi walishuhudia mwili wa marehemu ukiwa umewekwa
madhabahuni ;huku waumini wakiupapasa, wakiomba afufuke. Baadhi ya
waumini wa kanisa hilo, walisema Mchungaji Lwitiko aliwaongoza kwa mara
nyingine kuurejesha mwili wa marehemu ili uhifadhiwe chumba cha
kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa huku
wakisisitiza kuwa maombezi yaliyofanyika kanisani hapo ni ya imani yao.
Majirani walieleza umati mkubwa ulifurika katika uwanja wa kanisa
hilo, baada ya taarifa kuzagaa kuna marehemu anaombewa mwili wake ukiwa
madhabahuni, wakiamini atafufuka.
“Lakini walioruhusiwa kuingia kanisani kwa maombezi, lazima awe
muumini wa kanisa hilo na baada ya kuingia mlango wa kanisa ulikuwa
ukifungwa, “ alieleza mmoja wa waumini. Mwandishi wa habari hizi alifika
kanisani hapo jana asubuhi na kukuta milango imefungwa ;huku nyimbo
zikiendelea kuimbwa kanisani. Baadaye aliambatana na Mwenyekiti Mwazembe
na mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten kuingia kanisani kwa
mahojiano na mchungaji, lakini ndugu wa marehemu nusura wawapige,
wakidai hawakukaribishwa msibani. “Kwanza nyie nani... mmekuja kufanya
nini hapa ...ondokeni mara moja ....vinginevyo nendeni hospitali
mkaulize uzembe walioufanya na kusababisha kifo chake,” alifoka mmoja wa
wanandugu akitishia kuwapiga. Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Dk Halfany Haule
alisema anafuatilia tukio hilo na atatoa taarifa baadaye. Taarifa kutoka
kanisani hapo, zilieleza msiba huo upo Kitongoji cha Bangwe mjini
Sumbawanga.
No comments