Heade

KIGWANGALLA AWATAJA VIGOGO WATANO WALIOCHUKUA MAENEO NA KUJENGA KATIKA KIWANJA CHA NCAA



 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema vigogo watano ni miongoni mwa wanaotajwa kuwa ni kati ya watu 83 waliochukua maeneo na kujenga nyumba katika kiwanja cha Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Akizungumza na wajumbe wa bodi mpya ya NCAA aliyoizindua jana, Dk Kigwangalla alisema mwingine ni Daniel Ole Njoolay ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha, ambaye alisema ameshangazwa na madai hayo.

Aidha, Lowassa kupitia kwa mwanae, Fredrick ambaye ndiye msemaji wa familia amepangua tuhuma hizo huku Sumaye ambaye alikuwa waziri mkuu tangu mwaka 1995 hadi 2005, akisema atamburuza mahakamani Dk Kigwangalla kwa maelezo kuwa hana nyumba katika eneo hilo wala jijini Arusha.

“Nimewataja hawa baadhi, najua kuna wengine, sasa naipa jukumu bodi na menejimenti kuendelea kuwataja na hatua za kurejesha ardhi zianze,” alisema.

Waziri huyo alisema tayari ameshamueleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi juu ya mgogoro huo.

Alisema anajua njama zilizotumika kugawa eneo hilo la ekari 20 kati ya 40 kwa kuwa jiji la Arusha lilikuwa halina uwezo wa kugawa eneo ambalo si lake.

“Jiji wamegawa eneo hili mwaka 1996 wakati likiwa chini ya umiliki wa Shirika la Taifa la Utalii lililobinafsishwa na NCAA walinunua hili eneo mwaka 2006,” alisema.

Lakini, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Juliana Peter alisema walipata viwanja hivyo baada ya jiji kutangaza kuvigawa wakifuata taratibu zote, “Mzazi wangu ndiye alinunua kiwanja na najua ana hati hivyo sisi si wavamizi.”

Majibu ya Sumaye, Lowassa, Njoolay

Akizungumzia tuhuma hizo Sumaye huku akicheka alisema, “...Nitampeleka mahakamani. Nyinyi cha kufanya andikeni hicho alichokisema vizuri ili nimpeleke mahakamani. Sina nyumba yoyote Arusha sasa kama anadhani yeye kazi yake ni kuwachafua watu acha aendelee, nampeleka mahakamani.”

Fredrick katika ujumbe wake alioutoa mara baada ya baba yake kutajwa alisema, “Nimesikia taarifa za Kigwangalla akitaja jina la Lowassa kama mmoja ya watu eti walioshiriki kupora ardhi Arusha.”

Alisema amesikitishwa na matamshi hayo akisema hakutarajia kutolewa na mtu mwenye wadhifa wake.

Alisema Dk Kigwangalla anatumia vibaya dhamana aliyopewa na Rais John Magufuli kwa mambo ambayo Wizara ya Ardhi ina wataalamu wenye uwezo wa kuchukua hatua stahiki kwenye mgogoro wowote.

“Nikiwa kama msemaji wa familia ninazo katika kiganja cha mikono yangu taarifa zote za umiliki wowote unaomgusa Lowassa,” alisema, “Ninaweza kuuhakikishia umma kwamba yote aliyosema Kigwangalla hayapo na kama anayo basi sisi tuko tayari afanye lolote lililo chini ya mamlaka yake badala ya kurejea kule tulikopita ambako yeye na wenzake kadhaa walifanya bila mafanikio kuchafua heshima za wote anaowataja bila sababu.”

Baadaye waziri huyo alimjibu mtoto huyo wa Lowassa akisema, “Mdogo wangu Fredrick Lowassa, tulia usiwe na hofu. Sikukurupuka kuhusu issue ya mzee wako, Ndg. Edward Lowassa, kama ana kiwanja ama la, kwenye eneo la Plot No. 4091 Njiro Arusha.
Ukweli ni kwamba nilichokisema ni kuwa ‘tusubiri tupate majibu toka kwa mamlaka inayohusika na kutoa hati za umiliki wa ardhi kwa sababu kuna majina mengi makubwa yanasemwa... Hatuwezi kuwahukumu ama kuwataja waziwazi kwa sasa mpaka tupate nyaraka maana inawezekana wanasingiziwa.”

Njoolay, ambaye pia amewahi kuwa mkuu wa mikoa ya Mwanza na Rukwa alisema, “Nimesikitishwa sana na tamko la waziri. Niliwahi kuwa kiongozi serikalini, siwezi kuwa mvamizi kwa sababu Jiji lilitangaza viwanja na sisi tukaomba na kupatiwa kama wananchi wengine. Kigwangalla kama alitaka kupata ukweli angekutana na sisi kwanza. Akitaka kupata ukweli aunde kamati ndogo ambayo itabaini ukweli. Kusikiliza kabla ya kutuhumu ndio utawala bora. Tunajua Serikali haifanyi kazi kwa matamko kama suala hili lipo tunasubiri barua kutoka serikalini.”

Maagizo kwa bodi mpya

Mbali na kuitaka kufuatilia suala hilo la ardhi, Dk Kigwangalla ameitaka, “kusaidia kusimamia mali za NCAA lakini pia kuongeza siku za watalii kukaa Ngorongoro kutokana na kuongeza vivutio.”

“Pia mnapaswa kukaa na jamii kuboresha mahusiano ili ule mpango wa Ngorongoro wa miaka 10 ufanikiwe, hivyo mnapaswa kukaa na jamii kutafuta namna bora ya kujenga mahusiano kupitia miradi ya maendeleo,” alisema.

Agizo la Polisi palepale

Dk Kigwangalla alirejea agizo lake kwa Jeshi la Polisi kutaka liwakamate watuhumiwa wanne kwa madai ya kushiriki katika mtandao wa ujangili ndani ya siku saba.

Alitoa agizo hilo Januari 25 na kusisitiza kwamba jeshi hilo likishindwa kuwakamata, atalishtaki kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk Kigwangalla alisema jana kwamba anasubiri siku saba zifike na kama hatua zitakuwa hazijachukuliwa atafikisha suala hilo kwa Rais John Magufuli.

“Uamuzi wangu niliotangaza Januari 25 upo palepale nilitoa siku saba hazijafika ila zikifika kama hakuna hatua nitampelekea Rais jambo hili,” alisema.

Alisema ana imani kubwa na Polisi kuwa itazifanyia kazi taarifa alizotoa.

Hata hivyo, siku moja baada ya kutoa agizo hilo, msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa alisema halifanyi kazi kwa matamko, bali kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za kuanzishwa kwake.

Mwananchi lilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba kujua utekelezaji wa agizo la Waziri Kingwangalla alisema atafutwe Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro.

Hata hivyo, IGP Sirro alipopigiwa simu yake ya kiganjani hakupokea na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kuhusu utekelezaji wa agizo hilo hakuujibu.

No comments

Powered by Blogger.