KOREA KASKAZINI NA KOREA KUSINI ZAKUTANA KWA MAZUNGUMZO
Korea Kaskazini na Korea Kusini zimeanza mazungumzo ya kihistoria baada miaka 2 ya uhasama. Mazungumzo haya yanafanyika katika kijiji cha Panmunjom kuhusu uwezekano wa Korea Kaskazini kushiriki katika mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi yatakayofanyika Korea Kusini mwezi wa pili.
Uhusiano kati ya nchi hizi mbili ulidorora baada ya Korea Kusini kukatisha mradi wa pamoja wa kiuchumi katika eneo la kiuchumi la Kaesong nchini Korea Kaskazini, na kufuatiwa na majaribio ya nyuklia yaliofanywa na Korea Kaskazini.
Kijiji hicho hujulikana kama kijiji cha pande mbli, ambapo kila upande una miliki sehemu yake na katikati kuna jengo la umoja wa mataifa. Baada ya vita ya korea kuisha mwaka 1953 kijiji cha Panmunjom kiliamuriwa kuwa sehemu ya pande zote mbili, na maofisa wa pande zote mbili wanatarajiwa kukutana katika kijiji hiki.
Mazungumzo ya mwisho baina ya nchi hizo mbili yalifanyika Disemba mwaka 2015 nchini Korea ya Kusini.
Waziri wa Muungano wa Korea Kusini , Cho Myoung-Gyon amesema mazungumzo hayo yanajikita zaidi katika masuala ya olimpiki lakini mambo mengine pia yatajadiliwa ikiwa ni pamoja na kutumia fursa hiyo kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili hasimu.
Waziri Cho Myoung-Gyon ambaye ataongoza mazungumzo hayo amesema serikali yake itazungumzia pia suala la matokeo ya vita na njia za kupunguza mvutano wa kijeshi.
Korea Kaskazini imewakilishwa katika maungumzo hayo na maafisa watano wakiongozwa na Ri Son-gwon ambaye ni mwenyekiti wa Idara ya serikali ya Korea ya Kaskazini mwenye dhamana ya masuala na Kusini.
No comments