Heade

UTEUZI WA MAWAZIRI NCHINI KENYA UNA FIGISUFIGISU

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemuandikia Spika wa Bunge la nchi hiyo, Justin Muturi kumjulisha kuhusu uteuzi wa mawaziri watatu na Balozi ili wachunguzwe na kuidhinishwa au la.
Mawaziri hao ni John Munyes, Ukur Yattani na Keriako Tobiko. Aliyekuwa Msimamizi wa Ikulu, Lawrence Lenayapa ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Uholanzi.. Kabla ya uteuzi huo uliotangazwa Ijumaa iliyopita, Tobiko alikuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akajiuzulu saa kadhaakabla ya kuteuliwa kuwa Waziri. Munyes amewahi kuwa Seneta wa Turkana, na Yattani alikuwa Gavana wa Marsabit.
Wakati akitangaza mawaziri wapya, Rais Kenyatta alisema amekubali uamuzi wa Tobiko kujiuzulu na amewasilisha jina lake bungeni. Kwa kuzingatia utaratibu, Spika Muturi atawasilisha majina ya wateule kwenye Kamati ya Bunge ya Uteuzi na Kamati ya Bunge ya Ulinzi zenye wajibu wa kuchunguza mawaziri na mabalozi. Kwa mujibu wa Kanuni ya 45 (3) ya Bunge la Kenya, kamati hizo zinapaswa kuufahamisha umma kuhusu muda na mahali itakapofanyika mikutano ya kupokea hoja za wananchi kuhusu wateule hao.
Kamati hizo zinapaswa kuufahamisha umma angalau siku saba kabla ya kufanyika kwa mikutano hiyo. Kwa mujibu wa Kanuni ya 45 (4) ya Bunge la Kenya, kamati husika itafanya mkutano kupokea maoni ya wananchi kuhusu wateule na itawasilisha ripoti bungeni ndani ya siku 14 tangu Bunge lilipopokea majina ya wateule.
Hadi sasa Rais Kenyatta ametangaza kubakiza mawaziri sita tu waliokuwepo kwenye awamu ya kwanza ya uongozi wake na anatarajiwa kutawangaza wengine wakati wowote kuanzia sasa. Baada ya kutanganza uteuzi huo, Rais Kenyatta aliweka picha tatu akiwa na baadhi ya aliowateua kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter. Aliweka picha akiwa na Munyes, Yattani na Tobiko.
Hatma ya baadhi ya mawaziri walikuwa kwenye awamu ya kwanza ya uongozi wa Kenyatta haijulikani kwa kuwa hawakutajwa kwenye uteuzi wa Ijumaa kumsaidia Rais Kenyatta kutekeleza ajenda ya ‘Big Four’. Waziri hao ni pamoja na wa Mambo ya Nje, Dk Amina Mohammed, Rachel Omamo (Waziri wa Ulinzi), Mwangi Kiunjuri (Waziri wa Ugatuzi), Phyllis Kandi (Waziri wa Kazi), Judi Wakhugu (Waziri wa Mazingira) na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Eugene Wamalwa.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Willy Bett, Waziri wa Ardhi, Jacob Kaimenyi, Waziri wa Afya , Cleopa Mailu, Waziri wa Jinsia, Sicily Kariuki, Waziri wa Michezo, Ali Wario na Waziri wa Maendeleo ya Viwanda, Adan Mohamed. Viongozi hao wameagizwa kuendelea na kazi hadi mawaziri wapya watakapoapishwa.
Mawaziri waliokuwa kwenye awamu ya kwanza na wameteuliwa tena ni Henry Rotich (Wizara ya Fedha), Najib Balala (Utalii), James Macharia (Usafirishaji na Miundombinu) Fred Matiang’i, (Mambo ya Ndani na Mratibu Serikali ya Kitaifa na Kaimu Waziri wa Elimu).
Kabla ya uteuzi huo, Matiang’i alikuwa Waziri wa Elimu na Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani. Wengine walioteuliwa tena ni Charles Keter (Nishati) na Joe Mucheru (ICT). Kiongozi mwingine anayebaki kwenye Serikali ya Kenyatta ni Joseph Kinyua (Mkuu wa Utumishi wa Umma). Nzioka Waita ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Kitengo cha Rais cha Utekelezaji.

No comments

Powered by Blogger.