Heade

RAIS MAGUFULI AMESEMA WATOZA MICHANGO MASHULENI WACHUKULIWE HATUA

Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli ameagiza viongozi na watendaji ambao shule za msingi na sekondari katika maeneo yao zinawatoza wanafunzi michango mbalimbali kinyume na mwongozo wa Serikali wa utoaji wa elimu bila malipo wachukuliwe hatua kwa kukiuka taratibu hizo.
alitoa maagizo hayo jana Ikulu, Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Lazaro Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo kuhusu masuala hayo na mengine yanayohusu wizara wanazoongoza.
Katika mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana, Rais Magufuli alisema Serikali inatoa Sh bilioni 23.875 kila mwezi kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa elimu bila malipo lakini inashangaza kuona bado kuna walimu wanaendelea kuwatoza michango au kuwarudisha nyumbani wanafunzi ambao wanashindwa kutoa michango hiyo.
“Nawaagiza Mawaziri, sitaki kusikia mwanafunzi anarudishwa nyumbani kwa kushindwa kutoa michango, na fikisheni maagizo haya kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wote wanaohusika. Nikisikia tena mahali jambo hili linaendelea hawa niliowateua mimi wataondoka,” alisema.
“Haiwezekani tumefuta ada, halafu walimu wanaanzisha michango tena mikubwa ambayo watu masikini wanashindwa kusomesha watoto wao, na kama wazazi wanataka kuchangia kitu shuleni wapeleke michango yao kwa Mkurugenzi, lakini sitaki kusikia mwanafunzi anapewa sharti la kutoa mchango ndipo apokelewe shule,” alisema Rais Magufuli.
Alitoa maagizo hayo baada ya kupata taarifa kuwa zipo baadhi ya shule ambazo wanafunzi wanadaiwa michango mbalimbali tena kwa kiwango kikubwa ikiwemo chakula, maabara, madawati na ziara za kujifunza hali iliyosababisha wazazi kushindwa kumudu.
Kufuatia maagizo ya Rais Magufuli, Waziri Ndalichako aliwaagiza walimu na viongozi wa halmashauri kuwarudisha shule mara moja wanafunzi wote waliorudishwa nyumbani kwa kutotoa michango na kurejesha michango iliyokusanywa kinyume na mwongozo huo. Waziri Jafo naye aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwasilisha taarifa ya shule zilizotoza michango kinyume na mwongozo wa Serikali ifikapo Ijumaa wiki hii ili hatua zichuliwe dhidi ya walimu na maofisa elimu ambao wamekiuka mwongozo huo.
Katika hatua nyingine, Prof Ndalichako ameagiza Wakala wa Majengo (TBA) kuongeza kasi kwa kufanya kazi mchana na usiku pamoja na kuongeza mafundi ili kukamilisha ukarabati kwa shule za sekondari za Azania na Jangwani. Aliagiza utekelezaji huo ufanywe kwa haraka ili wanafunzi waweze kuanza masomo Jumatatu na mabweni na madarasa yakamilishwe Ijumaa.
Awali Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo alikuwa amesogeza mbele muda wa kufungua shule kwa shule tatu, Azania, Jangwani na Milambo kutokana TBA kushindwa kukamilisha ukarabati katika muda uliopangwa. Ulitakiwa kukamilika Januari 9. Akizungumza jana baada ya kutembelea shule za Jangwani na Azania, Prof Ndalichako alisema kasi ya kazi inakwenda vizuri lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya hivyo TBA, waangalie namna ya kuongeza mafundi zaidi.
“Jangwani na Azania ni shule kubwa, ujenzi bado unaendelea katika maeneo ya maabara majiko na hata eneo la mesi. Wafanye kazi mchana na usiku, na madarasa yakamilishwe angalau siku tatu kabla ya wanafunzi kuingia,” alisema Profesa Ndalichako baada ya kukagua.
Aliagiza TBA kuendelea na ujenzi kwa kasi na kuhakikisha eneo la madarasa na mabweni wanakamilisha mapema ili serikali isipate kesi za kiafya kwa wanafunzi watakaoingia shuleni.
Kuhusu kiwango cha fedha kinachotumika kwa ajili ya ukarabati alisema Shule ya Sekondari Azania imetumia Sh bilioni 1.4 huku Shule ya Sekondari Jangwani ikitumia Sh milioni 960. Mratibu wa Mradi wa ukarabati huo kutoka TBA, Cesilia Sospeter alisema Wakala huo unaahidi kutekeleza ukarabati ndani ya muda uliopangwa na kufanya kazi mchana na usiku.

No comments

Powered by Blogger.