Heade

TANZANIA NA RWADA ZIMEKUBALIANA KUJENGA RELI YA KISASA KUTOKA TANZANIA HADI RWANDA

TANZANIA na Rwanda zimekubaliana kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Isaka mkoani Shinyanga hadi mji Mkuu wa Kigali nchini Rwanda.
Hayo yalibainishwa na Rais John Magufuli na Rais wa Rwanda, Paul Kagame Ikulu, Dar es Salaam jana. Kagame yuko nchini kwaziara ya kikazi ya siku moja. Rais Magufuli alisema pamoja na mambo mengine waliyozungumza na Kagame, jambo moja kubwa ni kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili kwa kuanza ujenzi wa reli ya kisasa itakayokuwa na urefu wa zaidi ya kilomita 400 kati ya Isaka na Kigali.
Alisema kuwa shughuli za usanifu na upembuzi yakinifu zimeshakamilika na kikubwa kinachosubiriwa sasa ni kujua gharama halisi za mradi huo ili uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi ufanyike. “Tunawaagiza mawaziri wa miundombinu wa Tanzania na Rwanda mkutane ndani ya wiki mbili ili kujadili na kujua gharama inayotakiwa kwa mradi huu; suala la kupatikana kwa fedha za ujenzi mtuachie sisi (Magufuli na Kagame), tutajua kama tutakopa au tutatenga kupitia bajeti zetu,” alieleza Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutafungua milango ya biashara siyo tu kati ya Tanzania na Rwanda, lakini pia na nchi nyingine jirani kama vile Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Alisema kuwa Tanzania imeshaanza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora mkoani Dodoma yenye urefu wa Kilomita 726 kwa gharama ya Sh trilioni 7.6 ambazo ni fedha za Serikali.
Biashara Tanzania, Rwanda Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kuwa kiwango cha mizigo ya Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha mwaka jana ilikuwa tani 950,000 kiasi ambacho alisema kuwa kilishuka ikilinganishwa na miaka mingine. Aidha alisema hali ya biashara kati ya Tanzania na Rwanda kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 ilikuwa ikipanda na kushuka.
Alisema kwa mwaka 2011, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Rwanda ilikuwa Sh bilioni 106.54, mwaka 2012 Sh bilioni 27.34, mwaka 2013 Sh bilioni 132.21, mwaka 2014 Sh bilioni 64.45 na Mwaka 2015 ni Sh bilioni 83.95. Kwa upande wake, Rais Kagame alisema kuwa lengo la nchi hizo mbili ni kuwafanya wananchi wao kufanya biashara kwa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao, maendeleo yao binafsi pamoja na kudumisha amani.
“Nakuahidi Rais Magufuli, nitakuwa nakuja Tanzania mara nyingi kwa ajili ya kushauriana kwa mambo mbalimbali kwa faida ya nchi zetu na Afrika kwa ujumla,” alieleza Rais Kagame. Kagame kuwa Mwenyekiti AU Kuhusu Uenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais Magufuli alisema kuwa Tanzania inamuunga mkono Rais Kagame kwa nafasi hiyo ya uongozi anayotarajia kuishika hivi karibuni.
Alisema hana mashaka na Kagame kuimudu nafasi hiyo kutokana na uzoefu alionao wa kiuongozi. “Wewe ni mwanapinduzi wa kweli wa Afrika. Unajua mateso na umeyaishi mateso, umeishi ugenini kama mkimbizi, baadaye ukaja kuwa mtawala wa nchi, umeleta mabadiliko makubwa nchini Rwanda, naamini pia utaleta mabadiliko makubwa Afrika,” alieleza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais Kagame alisema kuwa Afrika inapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza shughuli za kibiashara na uwekezaji ili kuongeza ajira kwa vijana na kuwaondolea wananchi umasikini. Alisema pamoja na juhudi za serikali kuandaa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, lakini vijana wa Afrika wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo. Alisema kinachofanya serikali ni kuwawezesha vijana kielimu, kiujuzi na kuweka mazingira mazuri ili waweze kujitegemea.

No comments

Powered by Blogger.