Heade

TIZEBA SASA ATUA ZIGO LA MBOLEA KWA WAKUU WA MIKOA

WAZIRI wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amewaagiza wakuu wa mikoa, kusimamia usambazaji wa mbolea zinazoingia katika mikoa yao ili kuhakikisha zinawafikia wakulima vijijini kwa bei iliyopangwa na serikali.
“Nawaagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanisaidie katika kusambaza mbolea hii hadi vijijini ambako kilimo ndipo kinapofanyika, wakulima hawaishi makao makuu ya mikoa wala wilaya hivyo ipo haja ya kulisimamia hili la usambazaji,” alisema Dk Tizeba.
Aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuwa wafanyabiashara wasimamiwe ili wasiuze kinyume na bei elekezi, lakini pia hakuna sababu ya kuwaumiza wasafirishaji wakubwa kwa sababu na wao wanahitaji kupata faida.
Mapema mwaka jana, serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ilitangaza utaratibu wa kuagiza mbolea kwa pamoja na kuweka bei elekezi katika mbolea za kupandia na kukuzia, ambapo mbolea ya DAP haitakiwi kuuzwa zaidi ya Sh 56,000 na UREA isizidi Sh 48,000.
Aidha, bei hiyo elekezi kwa mujibu wa Dk Tizeba, inatofautiana na maeneo kulingana na umbali kutoka jijini Dar es Salaam. “Mbolea ipo ya kutosha kiasi cha tani 28,000 na ina uwezo wa kufika kwa wakulima wote msimu mzima, lakini ametoa angalizo kuwa lazima kuwepo na nidhamu ya kuisambaza ili iwafikie walengwa.

No comments

Powered by Blogger.