Heade

TUTAENDELEA KUVUTIA WAWEKEZAJI

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema serikali haitaacha kuweka sera, kanuni na taratibu za kushitukiza katika kusimamia sekta ya biashara nchini kwa vile wapo wafanyabiashara wasio waaminifu.
Amesema hata hivyo serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki zaidi ya kibiashara kwa wawekezaji ili kuwezesha nchi kupiga hatua za haraka kuelekea uchumi wa viwanda, utakaoipeleka nchi kuwa ya uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.
Dk Mpango amesema hayo mjini hapa jana katika kikao cha majadiliano ya pamoja baina ya serikali na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kukuza uchumi.
Katika hatua iliyoonesha serikali kutambua umuhimu wa sekta binafsi kama mdau muhimu katika kukuza uchumi, mawaziri na naibu mawaziri zaidi ya 10 walishiriki, huku Dk Mpango, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na Naibu Waziri wa Nishati, Stanslaus Nyongo wakiwa walengwa wakuu.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte alisema miongozo, sera, kanuni na operesheni za kushitukiza zinazofanywa na serikali katika kushughulikia masuala ya biashara, zinarudisha nyuma uwekezaji kutokana na wafanyabiashara kutofahamu nini kitatokea kesho.
Alisema ili wafanyabiashara wawekeze mitaji mikubwa hasa wakati huu ambao serikali imejielekeza katika kuhamasisha ukuaji wa uchumi wa viwanda, ni lazima wawe na uhakika wa nini kitatokea kesho ili kulinda mitaji na uwekezaji wao.
Akijibu, Dk Mpango alisema ni vigumu kwa serikali kuondokana na mtindo huo wa kushughulikia udhibiti wa masuala ya kibiashara, kwa vile wapo wafanyabiashara ambao si waaminifu na wamekuwa wakiibia serikali na Watanzania mali zao na kupeleka nje.
Alisema ili kuwadhibiti wafanyabiashara wa aina hiyo ambao wamekuwa wakiibia nchi na kupoteza ushahidi kwa haraka ili wasikamatwe, serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kushitukiza ili kuwadhibiti na kuokoa fedha na rasilimali za Watanzania.
Hata hivyo, alisema serikali inatambua umuhimu wa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini na imekuwa inachukua hatua hizo kama vile kuharakisha utoaji wa uamuzi, kujenga mazingira mazuri, kuangalia upya mfumo wa kodi na pia kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo bandari na reli.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante ole Gabriel alisema serikali imeanza kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kujielekeza zaidi katika ukuzaji wa uchumi wa viwanda na sekta binafsi ni mdau muhumi.
Alisema katika kufikia lengo hilo, serikali imeanza kusimamia mikakati ya kuhakikisha viwanda vyote vilivyopo nchini, vinafanya uzalishaji kwa uwezo wake wote, kuvifanya kuwa na uzalishaji wenye tija, kuhamasisha na kuwezesha wafanyabiashara Watanzania wanapata fursa ya kuwekeza kwenye viwanda.
Mikakati mingine ni kuhamasisha wawekezaji wakubwa wa nje, kuwekeza katika viwanda mbalimbali katika ngazi ya Kanda na Taifa na kwamba katika kuwavutia ndio maana serikali inachukua hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu ikiwemo ya bandari na reli.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Andrew Charles alisema serikali na sekta binafsi ni sawa na pande mbili za sarafu. Alisema kama pande hizo mbili zikishirikiana vizuri, ukuaji wa uchumi utakwenda sambamba na ukuaji wa maendeleo ya jamii

No comments

Powered by Blogger.