Heade

UDHIBITI WA MAUDHUI SIYO KUMINYA UHURU WA HABARI

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema hatua ya kudhibiti maudhui katika vituo vya utangazaji si kuminya uhuru wa habari bali kulinda mtumiaji wa huduma za mawasiliano na kujenga taaluma.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Mwongozo kwa Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano. Dk Mwakyembe alisema chombo cha habari ambacho kinafuata maadili kinajenga heshima ya kituo na weledi wa wanahabari na kuwa kinyume chake kinaleta taswira mbaya hivyo kusisitiza watoa huduma kuhakikisha wanatoa huduma kwa kuzingatia sheria za utangazaji na maudhi yenye maadili.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa elimu kwa wananchi ya namna ya kufikisha malalamiko wanapopatiwa huduma zisizostahihi kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano ili kupata haki zinazostahili.
“Ili tuweza kukabiliana na changamoto mamlaka inatakiwa kuwahimiza watoa huduma namna ya kuzingatia kanuni na sheria kwa kuwafuatilia kama wanatekeleza na kutoa elimu iliyo nyepesi kwa wananchi,” alieleza.
Aidha, Nditiye amezitaka mamlaka zinazohusika kuzuia matangazo ambayo wananchi hawayapendi sambamba na kampuni za ving’amuzi zilizokaidi kutoa chaneli tano za bure kama serikali ilivyotoa maelekezo.
Pia Nditiye aliipongeza TCRA kwa kupunguza gharama za mwingiliano wa simu kutoka Sh 34.9 mpaka Sh 15.6 kwa dakika na kutaka punguzo hilo lionekane kwa kupungua kwa gharama kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema lengo la kuandaa mwongozo huo ni kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi kuhusu huduma za mawasiliano wazipatazo kutoka kwa watoa huduma.
Alisema chimbuko la mwongozo huo ni maswali mengi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano na kuwa kitabu hicho kinakuja kujibu maswali na kuahidi itakisambaza kote nchini ikiwa ni pamoja na vyuoni na shuleni.

No comments

Powered by Blogger.