Heade

AG MPYA AANIKA VIPAUMBELE VYAKE

Uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli wa mtalaamu mbobezi wa sheria za mafuta na gesi, Dk Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) umewakuna wengi.
Dk Kilangi mwenyewe ameahidi kutekeleza majukumu yake hayo kwa uaminifu unaotakiwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwenye sekta ya sheria nchini. Dk Kilangi aliahidi hayo wakati akizungumza na gazeti hili jana akiwa safarini akitokea mkoani Tabora kwenda Mwanza kupanda ndege ili awahi kuapishwa leo saa 9:00 alasiri Ikulu jijini Dar es Salaam.
Juzi Rais Magufuli alimteua Dk Kilangi kushika wadhifa huo, badala ya George Masaju ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Katika uteuzi huo wa juzi, pia Rais Magufuli alimteua Paul Ngwembe kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG) huku aliyekuwa na wadhifa huo, Gerson Mdemu naye akiteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Kabla ya uteuzi wake, Dk Kilangi alikuwa Mkurugenzi wa Tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Tawi la Arusha, ambako alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Sheria za Kimataifa, Nadharia, Madini na Mafuta.
Ngwembe alikuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA). Dk Kilangi aliliambia gazeti hili kuwa ameupokea uteuzi huo kwa heshima kubwa na kuwa atashirikiana na wadau wa sheria katika kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaimarika zaidi kwa kuzikabili changamoto zake zote.
Naye Ngwembe alisema huo ni uteuzi wa imani ambayo Rais ameonesha kwao na kuwa atahimiza zaidi utendaji wa kazi kama timu moja hasa katika kukabiliana na changamoto kwenye sekta hiyo kwa kubuni mbinu mbadala.
Alisema atashirikiana na mwanasheria mkuu katika kuhakikisha kuwa wanapatikana wataalamu wengi zaidi kwenye sekta hiyo ambao watashiriki katika kutatua kero za watu hususan kwenye nyanja za sheria.
Aliongeza kuwa, suala la mikataba nalo halitafumbiwa macho kwa kuwa mikataba mingi inahitaji ushiriki wa ofisi hiyo katika kutoa ushauri na mwelekeo stahiki kwa mustakabali wa nchi.
Uteuzi huo umeonekana kuwagusa watu wengi zaidi hasa kwenye sekta ya sheria ambao wamewazungumzia wawili hao hasa kwa kuonesha imani yao kwao katika kuimarisha sekta hiyo nyeti nchini.
Dk Onesmo Kyauke, alisema Rais Magufuli ameteua watu makini na wenye weledi wa juu katika masuala ya sheria na kuwa na mwito mkubwa kwenye kazi hizo. Aliongeza anamfahamu zaidi Dk Kilangi kwa kuwa alikuwa mwanafunzi mwenzake kwenye masomo ya sheria Chuo Kikuu Dar es Salaam (Udsm) ambako alimsifia kuwa ni mtaalamu katika sheria ya gesi na mafuta rasilimali ambayo kwa sasa ni muhimu.
“Huyu ni mtalaamu mbobezi kwenye sheria na mafuta na gesi, sasa uteuzi huu umekuja kwa wakati mzuri ambapo nchi inaanza kuona neema ya rasilimali hizo muhimu kwa nchi, kwa kuwa huyu anakuwa sasa kiungo muhimu kwenye mikataba ya nchi na kampuni za madini hivyo basi Rais amemteua mtu muhimu sana,” alisema Dk Kyauke.
Alisema moja kati ya sifa kubwa ya Dk Kilangi ni mtu mwenye kiwango cha juu cha uadilifu na hivyo ataweza kukabiliana na mianya ya rushwa ambayo imekuwa ikiathiri sekta mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Wakili wa muda mrefu nchini, Profesa Costa Mahalu alisema Dk Kilangi siyo tu mtaalamu katika nyanja za sheria za kimataifa, bali hata kwenye nyanja za ndani ya nchi huku akimweleza ni mkongwe kwenye sheria za mafuta na gesi.
Profesa Mahalu alisema: “Rais Magufuli amemteua mtu ambaye hakika atakuwa akimshauri mengi katika nyanja mbalimbali na kwenye sekta ya mafuta na gesi na ni imani yangu kuwa mtu wa kazi amepata mtu wa kazi.”
Lakini hata hivyo, Mahalu aliwatoa hofu watu wanaodhania Dk Kilangi hakuwahi kufanya kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu anaweza kukabiliwa na changamoto kadhaa kwenye utendaji wake, kwa kuwataka watambue kuwa Dk Kilangi ni mtu mwelewa na mwenye uwezo wa kazi.
Wakili Alex Mgongolwa aliwataja wawili hao kuwa ni watu wenye historia nzuri kwenye kazi zao na hasa kutokana na matokeo chanya yaliyojitokeza kwenye utendaji wao wa kazi kwenye sekta mbalimbali.
Zaidi, wapo wataalamu wengine wa sheria ambao hawakutaka kutaja majina yao wamesema kuwa, mwanasheria mkuu huyo na naibu wake kama wakizingatia miiko ya kazi zao na wasishawishike kupendelea mambo ya kiserikali zaidi, wanaweza kufanya vema.
Walimtaka Dk Kilangi kutambua kuwa kutokana na wadhifa wake huo anakuwa Mbunge atakayewakilisha serikali na kuwa anatakiwa kutenda haki kwa watu wa vyama vyote vya siasa katika kusikiliza na kufafanua hoja na siyo kuwa zaidi kwa maslahi ya serikali hata kwa mambo yenye kuhitaji kutumika kwa weledi wake.
Dk Kilangi mbali na kuwa mtaalamu wa sheria za mafuta na gesi, pia ni mtaalamu wa sheria za kimataifa na za ukanda pia huku akiwa amefanya kazi kama Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Sheria za Kimataifa katika Umoja wa Afrika (AU) kuanzia mwaka 2009 hadi 2015.
Alikuwa na jukumu la kuwashauri wakuu wa nchi za Afrika na Kamati za Umoja wa Nchi za Afrika kuhusu masuala ya sheria za kimataifa. Pia amewahi kufanya kazi kama Mshauri wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya sheria za madini.
Alisaidia upatikanaji wa sheria mpya za madini nchini Lesotho. Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kituo cha Maendeleo ya Katiba kwa Afrika Mashariki. Dk Kilangi ni Mwanasheria Mkuu wa Tisa, akitanguliwa na AGwas Roland Brown kuanzia mwaka 1964 hadi 1965, alifuatiwa na Jaji Mark Bomani mwaka 1965 hadi 1976 kisha kuja Jaji Joseph Warioba mwaka 1976 hadi 1985.
Jaji Warioba alimwachia Jaji Damian Lubuva kuanzia mwaka 1985 hadi 1993 kisha akachukua Andrew Chenge hadi mwaka 2005 aliyekuja kumwachia Johnson Mwanyika mwaka 2005 hadi 2009.
Jaji Frederick Werema alichukua kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 ambapo hapo alikuja kuchukua wadhifa huo Masaju aliyedumu kwa miaka mitatu, na sasa ameingia Dk Kilangi.

No comments

Powered by Blogger.