Heade

WAZIRI ANASA KONTENA 5 ZA MWANI ZIKITOROSHWA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amekamata makontena matano yenye tani 100 za zao la mwani yenye thamani ya Sh bilioni 1.4 katika Bandari ya Dar es Salaam yakiwa tayari kwa ajili ya kutoroshwa kwenda Ufaransa huku mmiliki wa mzigo huo akiwa hana kibali wala leseni ya kusafi risha mazao hayo ya uvuvi kwenda nje ya nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mpina alisema tayari serikali imeshaomba kibali cha Mahakama ili kuwezesha tani hizo za mwani kuuzwa kwa njia ya mnada baada ya mmiliki wake Kampuni ya Mari Culture kutojitokeza kwa zaidi ya wiki moja sasa tangu mzigo huo ulipokamatwa.
Mpina alisema Mari Culture imekiuka kifungu namba 65(1) cha Sheria ya Mazingira kwa kutaka kutorosha mazao ya uvuvi bila kuwa na vibali vilivyoainishwa ambapo kwa kuzingatia makosa hayo, imetozwa faini ya Sh milioni 100 kama Kipengele namba 191 cha Sheria ya Mazingira Namba 20 ya Mwaka 2004 kinavyoelekeza.
Aidha, alisema serikali inahamasisha ukuaji wa shughuli za kilimo cha mwani na ndio maana hata taasisi zake ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) zimekuwa zikifadhili mafunzo kwa wakulima ili kuchochea uchumi wao na Taifa kwa ujumla, lakini haitavumilia wafanyabiashara wanaotumia njia za mkato kusafirisha mazao hayo.
Hata hivyo alisema kitendo cha kukwepa kutumia vibali vya serikali kimesababisha Taifa kupoteza mapato mengi yatokanayo na zao hilo huku ikichangia kuikosesha serikali takwimu sahihi zitokanazo na zao hilo linalotegemewa na wananchi wengi wa ukanda mzima wa Pwani ya Bahari ya Hindi.
Pia Mpina amewaonya wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi wanaondelea kufanya kazi hiyo bila ya kuwa na leseni watambue kuwa watasakwa na kukamatwa kwani Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli iko makini katika kusimamia rasimali za uvuvi zilinufaishe Taifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwanaidi Mlolwa alisema mmiliki wa mwani huo hakuwa na kibali cha kuchakata zao hilo wala leseni ya kusafirisha nje ya nchi ambapo ni kinyume cha Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009.
Alisema Kanuni ya 13(1) kipengele (a-c) inaelekeza kuwa mtu yeyote haruhusiwi kukusanya, kumiliki au kusafirisha mazao ya uvuvi kwa dhumuni la biashara bila kuwa na leseni halali inayomruhusu kufanya biashara hiyo ambapo mtu yeyote anayetaka kufanya biashara hiyo kwa kuzingatia vifungu hivyo.
Pia alisema mtu yeyote haruhusiwi kusafirisha nje ya nchi mazao ya uvuvi bila kuwa leseni hai iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uvuvi inayomruhusu kufanya biashara hiyo ambapo pia mtu au kampuni inayofanya biashara ya mazao ya uvuvi inatakiwa kuwasilisha marejesho kama kanuni namba 71(2) inavyoelekeza.
Mlolwa alisema kutokana na kifungu namba 65(i) cha Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004 kinachotaka rasilimali zisimamiwe kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 na kanuni zake na kwamba kampuni hiyo imekiuka kifungu namba 65(i) cha Sheria ya Mazingira kwa kutaka kutorosha mazao ya uvuvi bila ya kuwa na vibali vinavyotakiwa kisheria

No comments

Powered by Blogger.