Heade

MADARAJA 79 KUJENGWA RUKWA

Serikali imeutengea Mkoa wa Rukwa zaidi ya Sh bilioni 13.8, zitakazotumika kukarabati barabara kuu za mkoa zenye umbali kilometa 905.93 na ujenzi wa madaraja 79 kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Rukwa, Msuka Mkina alisema, mpango kazi wa matengenezo ya barabara za mkoa, zaidi ya Sh bilioni 10.8 zitatumika kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 552.39 na madaraja 52.
Zaidi ya Sh bilioni tatu zitatumika kukarabati barabara kuu zenye urefu wa kilomita 333.54 na madaraja 27. "Mkoa wa Rukwa una mtandao wa barabara zenye umbali wa kilomita 1,210.60 unaosimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Tanroads, katika mtandao huu barabara kuu zina umbali wa kilomita 407.94 huku barabara za mkoa zina urefu wa kilomita 802.66,”alieleza.
Aliongeza kuwa, kutokana na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambao unaendelea, kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 305.26, kimeshakamilila kwa kiwango cha lami ambapo kilomita 252.95 ni za barabara kuu na kilomita 52.31 ni za barabara za mkoa.
Barabara zilizo katika hali nzuri ni zenye urefu wa kilomita 632.30 sawa na asilimia 69.84, huku zilizo katika hali ya wastani ni kilomita 269.36 sawa na asilimia 29.75 na zilizo katika hali mbaya ni kilomita 3.68 sawa na asilimia 0.41.

No comments

Powered by Blogger.