Heade

MFUMO TRA KUUNGANISHWA NA BIMA ZA MIZIGO

Mfumo wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwezi huu unatarajiwa kuunganishwa na mfumo wa kuuza na kununua bima za mizigo, itakayotoka nje ya nchi (TIIP).
Hatua hiyo inaweza kuinufaisha nchi kutokana na mizigo au bidhaa kutoka nje, zilizowekewa bima kwa maana ya kuongezeka kwa mapato ya bima na kodi husika.
“Kwa dhati ninaomba kuunganishwa kwa mfumo wa forodha wa TRA na tuna matumaini kwamba jambo hilo litakamilika kabla ya mwisho wa mwezi huu,” amesema Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) nchini, Dk Baghayo Saqware.
Katika taarifa yake kwa gazeti hili jana, Dk Saqware aliwahimiza TRA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wadau wengine kuutumia mfumo huo aliouita wa dirisha moja.
Alisema kuwa mfumo huo kupitia tovuti ya www.tiip.co.tz, unawapa fursa wasafirishaji wa bidhaa nje ya nchi kupata huduma ya bima kwa njia ya mtandao saa 24 kwa wiki kwa mwaka mzima na wanaweza kufanya malipo kwa njia ya mtandao kwa kuchagua kampuni ya bima ya ndani aliyojisali nayo. Kwa mujibu wa Dk Saqware, mfumo huo unarahisisha kuwepo kwa eneo moja la kufanyia miamala ya uagizaji wa bidhaa nchini.
Akizungumzia faida za kutumia TIIP, alisema kuwa Watanzania na makampuni ya Tanzania yanaweza kukua na hivyo kuachana na mazoea ya kusafirisha fedha nje ya nchi.
Alisema kuwa TIRA inaona matumizi ya mfumo huo, utainufaisha nchi kutokana na ukusanyaji wa kodi inayotokana na makampuni yaliyoko kwenye sekta ya bima, lakini pia kodi ya ongezeko la thamani (VAT) nayo itaongezeka kwa upande wa TRA.
Kamishna huyo aliongeza kuwa hatua hiyo, pia itaiwezesha sekta ya bima kuwa imara na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi.
Dk Saqware alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti, uliofanyika kuanzia mwaka 2009 hadi 2013, Tanzania imekuwa ikipoteza wastani wa dola 2,000,000 kila mwezi kwa kuruhusu bima ya kigeni kupitia mizigo inayoletwa kwa njia ya bahari.
Alisema kwa takwimu za kipindi hicho hicho pia zinaonesha kuwa waagizaji bidhaa wa Watanzania, wamesafirisha nje ya nchi kwenye masoko ya bima ya nje zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja.

No comments

Powered by Blogger.